MAFUTA na gesi asilia ni rasilimali ambazo zimekuwa mkombozi kwa mataifa mengi ya Afrika ingawa mataifa ya Magharibi yamekuwa yakinufaika zaidi kuliko hata nchi zilizo na rasilimali hizo.
Utafiti ambao umefanywa na mtandao wa www.fikrapevu.com unaonesha kuwa,hali hiyo inatokana na ukweli kwamba, rasilimali hizo, kama ilivyo kwa madini, zimeanza kutafutwa na mataifa ya Ulaya tangu bara hilo likiwa bado linatawaliwa na wakoloni ambao wana utaalamu kuliko nchi za Afrika.
Licha ya kuwa na wataalam wachache, lakini mataifa ya Afrika yenye kuzalisha mafuta na gesi yameweka misingi ya kusimamia rasilimali hizo ikiwemo sheria na kanuni mbalimbali.Tanzania, kama miongoni mwa nchi zenye rasilimali hizo, imeweka taratibu za kusimamia mafuta na gesi asilia ambayo mpaka sasa imegundulika kiasi cha futi za ujazo trilioni 57.
Sheria hizi karibu zinafanana katika kila nchi ambapo kuna makundi mawili ya sheria hizo ambapo zipo zilizoandikwa na zipo ambazo hazijaandikwa, lakini zote zikiwa na malengo ya kulinda rasilimali za taifa. Sheria zilizoandikwa zinahusisha Katiba ya nchi, Sheria za kawaida (statutory laws), sera, kanuni, na mikataba.
Kuna uhusiano mkubwa baina ya Katiba, sheria, kanuni na mikataba. Miradi ya mafuta na gesi asilia inajikita Zaidi kwenye mikataba ambayo inawahusisha washirika wote kama Kampuni za Mafuta za Taifa (NOC), kampuni za mafuta za kimataifa (IOC), wakandarasi, wakandarasi wadogo, benki ambazo hutoa mikopo kugharamia miradi ya utafiti na uzalishaji, kampuni zinazotoa huduma, pamoja na wadau wengine.
Miongoni mwa mikataba hiyo, Mkataba wa Serikali Mwenyeji (Host Government Agreement – HGA au HGC) ndio wa kwanza kabisa, ambao unaiunganisha serikali na kampuni ama kundi la kampuni.
Mara nyingi mkataba huo unajulikana kwa majina mengi kama vile; Mkataba wa Mafuta (Petroleum Contract); Mkataba wa Utafiti na Uzalishaji (Exploration & Production Agreement – E&P); Mkataba wa Utafiti na Matumizi (Exploration & Exploitation Contract); Mkataba wa Leseni (License Agreement); Mkataba wa Uzalishaji wa Pamoja (Petroleum or Production Sharing Agreement – PSA).
Mikataba mbalimbali ya serikali inaweza kugawanywa katika makundi kama Mkataba wa Maridhiano (Concessional Agreement), Mikataba ya Uzalishaji wa Pamoja (Production Sharing Contracts), Mikataba ya Huduma (Service Contracts), na Mikataba ya Ubia (Joint Venture Agreements).
Mkataba wa Maridhiano ni utaratibu wa maridhiano yanatoa sehemu ya ardhi, na rasilimali zilizo chini ya ardhi zikijumuishwa, kwa kampuni, ili kama kampuni itagundua mafuta kwenye kipande cha ardhi, inamiliki mafuta hayo.
Makubaliano ya Kuchangia Uzalishaji ni uzalishaji wa pamoja baina ya serikali mwenyeji kupitia kampuni ya taifa inayosimamia mafuta na gesi na kampuni ya kimataifa, na hayampi mkandarasi umiliki wa mafuta yalioko ardhini; umiliki wa rasilimali unakuwa kwa dola.
Mpangilio mwingine, ambao mara nyingine huchukuliwa kama ni aina ya nne ya mipangilio ya kimkataba, ni ubia (Joint Venture), ambao unahusisha dola kupitia kampuni ya taifa ya mafuta, kuingia ubia na kampuni au kikundi cha kampuni za mafuta. Ubia wenyewe katika hali hii unapewa haki ya kutafiti, kuendeleza, kuzalisha na kuuza mafuta.
Kwa ujumla, mikataba yote hiyo lazima iendane na sheria zilizopo katika nchi husika ikionesha utangulizi, tafsiri, haki ya kisheria, mtazamo wa jumla, haki za msingi, majukumu na wajibu.
Mikataba hiyo kwa mujibu wa sheria, inatakiwa kuwa na usiri, kipengele cha kikomo, kipengele ya kusitisha, kipengele cha kuhusisha usuluhishi ikiwa upande mmoja utakiuka masharti ama kuona unaonewa, na uwezekano wa kuhamisha kwa mwingine.
Inafahamika kwa mafuta au gesi haidumu milele kwa sababu ni rasilimali isiyohuishwa kama ilivyo kwa madini, hivyo mikataba mingi inaandaliwa kwa kuzingatia uhai wa mradi wenyewe (life span of a project) tangu kuanza kwake, katikati kwenye uzalishaji na hadi mwisho kwenye usambazaji.
Maana yake hapa ni kwamba, lazima kuazingatia vipengele vinne ambavyo ni utafiti, uendelezaji, uzalishaji, na kuutelekeza wakati uhai wake unapokoma.
Utafiti unafanyika ili kutambua kama kuna rasilimali husika na taarifa zinazokusanywa zinapangwa katika makundi 10 tofauti ya mizania ambapo alama sufuri inamaanisha kwamba hakuna uhakika kabisa; alama 1-3 maana yake ni kwamba hakuna uhakika; alama 3-5 maara yake hakuna uhakika sana; alama 5-7 maana yake kuna uhakika; alama 7-9 inamaanisha uhakika mkubwa; na alama 10 maana yake rasilimali hiyo ipo au imegundulika.
Makala haya yameandikwa na Albano Midelo
mawasiliano albano.midelo@gmail.com,simu 0784765917
SONGEA MUNICIPAL COUNCIL
Anuani ya Posta: P O BOX 14, SONGEA
Simu ya Mezani: 025 2602970
Simu ya Kiganjani:
Barua Pepe: info@songeamc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Manispaa ya Songea. Haki zote zimehifadhiwa