Na,
AMINA PILLY,
AFISA HABARI MANISPAA.
24 Desemba 2021.
Halmashauri ya Mji wa Mbinga yakamilisha ujenzi wa vyumba vya madarasa 39 na kuyakabidhi rasmi kwa Mkuu wa Wilaya ya Mbinga Aziza Ally Mwangasongo hapo jana tarehe 23 Desemba 2021.
Ujenzi wa madarasa hayo ambayo yamekamilika na kukabidhiwa kwa Mkuu wa Wilaya ya Mbinga ni utekelezaji wa mpango wa maendeleo kwa ustawi wa Taifa na mapambasno dhidi ya UVIKO-19 kwa lengo la kutatua changamoto ya miundombinu ya elimu katika shule za sekondari pamoja na vituo shikizi kwa shule za msingi.
Mwangasongo amempongeza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji wa Mbinga pamoja na wataalamu kwa usimamizi bora wa miradi hiyo ambapo hadi sasa miradi hiyo imekamilika kwa asilimia 99% katika viwango vyenye ubora unaotakiwa.
Alisema kuwa ujenzi wa madarasa hayo pamoja na uboreshaji wa miundombinu ya elimu ikiwemo na samani (viti na meza) utasaidia kupunguza na kumaliza kabisa changamoto za mikundombinu pamoja na utoro kwa wanafunzi na kuongeza idadi ya wanafunzi watakaofanya vizuri zaidi katika kipindi kijacho cha masomo.
Amewataka wazazi na walimu kuhakikisha watoto waliochaguliwa kujiunga na masomo ya sekondari kwa mwaka 2022 wanaripoti shuleni kwa wakati kwa kuwa changamoto ya upungufu wa vyumba vya madarasa imeshatatuliwa.
Alisema “Miradi hiyo imeleta dira na muongozo wa kuendelea kutumia mfumo wa ujenzi uliotumika katika kutekeleza ujenzi wa vyumba vya madarasa 39 katika miradi mingine ambayo itatekelezwa katika Halmashauri hiyo”Mwangasongo Alisisitiza.
Ametoa rai kwa walimu pamoja na wanafunzi kusimamia na kutunza miundombinu hiyo na kuhakikisha inabaki katika ubora unaotakiwa ili madarasa hayo yaweze kutumika kwa vizazi vijavyo.
Naye Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji wa Mbinga Grace Quintine alibainisha kuwa Halmashauri ya Mji wa Mbinga ilipokea kiasi cha shilingi Milioni 860 kwa ajili ya ujenzi wa vyumba vya madarasa 39 na bweni moja ambapo vyumba vya madarasa 34 kwa shule za Sekondari na vyumba vya madarasa 5 kwa vituo shikizi 2 vikiwemo na kituo cha Mpepai pamoja na Kipungu.
Alieleza kuwa utekelezaji wa miradi hiyo ulitegemea mikakati mbalimbali iliyowekwa ikiwemo na kufanya kikao na wakuu wa shule,kamati za ujenzi na wahasibu kwa lengo la kujadili na kujipanga namna ya utekelezaji wa miradi hiyo kwa wakati stahiki, uandaaji na ufungaji wa mikataba na mafundi walioshinda zabuni ya ujenzi wa madarasa hayo, kutoa mafunzo kwa kamati ya force akaunti za kamati ya ujenzi, manunuzi, mapokezi na ukaguzi pamoja na kuunda kamati ya ufuatiliaji wa mradi huo ndani ya Halmashauri.
Akibainisha baadhi ya shule zilizonufaika na mradi huo ni pamoja na shule ya sekondari Luhuwiko vyumba vya madarasa 2, Mbambi Sekondari madarasa 2, Lamata Sekondari madarasa 2, Makita Sekondari madarasa 2, Ngwilizi Sekondari madarasa 2, Mbangamao Sekondari madarasa 3 pamoja na Usetu Sekondari madarasa 2 nanyinginezo.
Miongoni mwa changamoto zilizojitokeza katika kipindi cha utekelezaji wa mradi huo ni pamoja kupanda kwa gharama za vifaa vya ujenzi ikiwemo na nondo na bati, uhaba wa vifaa vya ujenzi baada ya kuongezeka kwa uhitaji wa vifaa hivyo katika maeneo mbalimbali ambapo katika kukabiliana na changamoto hizo Halmashauri iliagiza vifaa moja kwa moja kutoka kiwandani”Alibainisha”.
Quintine alimshukuru Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Mkuu wa Wilaya ya Mji wa Mbinga, Mbunge wa Jimbo la Mbinga Mji, wataalamu kutoka Halmashauri ya Mji wa Mbinga pamoja na wakuu wa shule kwa usimamizi mzuri wa miradi hiyo na kufanikiwa kukamilika kwa muda muafaka uliopangwa na Serikali.
Akizungumzia utoaji wa mikopo kwa vikundi inayoratibiwa na kusimamiwa na maendeleo ya jamii Halmashauri ya Mji wa Mbinga alisema “Halmashuri ya Mji wa Mbinga imetoa mkopo wa Zaidi ya shilingi milioni 100 kwa vikundi 28 vya wanawake 4%, vijana 4% na watu wenye mahitaji maalumu 2% ambao walikabidhiwa hundi ya fedha hizo chini ya usimamizi wa Mkuu wa Wilaya ya Mbinga iliyoambatana na zoezi la ugawaji wa mbegu za alizeti kwa vikundi mbalimbali vya ujasiriamali zilizonunuliwa kwa fedha za mapato ya ndani ya Halmashauri pamoja na ugawaji wa vitalu vya kahawa kwa wanakikundi kwa lengo la kuinua kipato chao na uchumi na Taifa kwa ujumla.
Mwisho.
SONGEA MUNICIPAL COUNCIL
Anuani ya Posta: P O BOX 14, SONGEA
Simu ya Mezani: 025 2602970
Simu ya Kiganjani:
Barua Pepe: info@songeamc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Manispaa ya Songea. Haki zote zimehifadhiwa