Halmashauri ya Manispaa ya Songea imejipanga kutatua changamoto za miundombinu ya barabara, umeme na maji kwa wananchi wake.
Hayo yameelezwa katika kikao cha Baraza la Madiwani Halmashauri ya Manispaa ya Songea kilichofanyika tarehe 30 Septemba 2021 katika ukumbi wa Manispaa ya Songea na kuhudhuriwa na viongozi pamoja na wataalamu mbalimbali ndani ya Manispaa ya Songea.
Akiongoza kikao hicho Naibu Meya wa Manispaa ya Songea Jeremiah Milembe katika kipindi cha maswali na majibu ambapo Waheshimiwa Madiwani walieleza changamoto mbalimbali zinazowakabili wananchi katika maeneno yao hasa miundombinu ya barabara , umeme na maji ambapo miongoni mwa changamoto hizo ni pamoja na ubovu wa barabara za mitaa, ukataji wa umeme mara kwa mara pasipo kutoa taarifa maalumu kwa wananchi, kucheleweshwa kwa uingizaji wa umeme pamoja na ukataji wa maji kwenye maeneo mbalimbali bila taarifa.
Akijibu malalamiko hayo Mhandisi mipango TANESCO Mkoa wa Ruvuma Eng. Sosthenes Maganga alisema kuwa sababu zinazopelekea ucheleweshwaji wa miundombinu ya umeme kwenye makazi ya wananchi pamoja na taasisi za umma na binafsi ni ukosefu wa bajeti ya kutosha ili kukamilisha miradi hiyo na upungufu wa nguvu kazi.
Maganga ametoa rai kwa viongozi wa Halmashauri ya Manispaa ya Songea kutoa taarifa mapema TANESCO mara tu utekelezaji wa miradi unapoanza ili kurahisisha upelekaji wa miundombinu ya umeme mapema kwenye miradi hiyo.
Kwa upande wake kaimu meneja TARURA Manispaa ya Songea Dotto Magese amesema kuwa wamejipanga kutengeneza barabara zote zenye changamoto ndani ya Manispaa ya Songea pamoja na kuweka utaratibu maalumu wa kuwashirikisha viongozi hasa Madiwani wa eneo husika ambalo utengenezwaji wa barabara utakuwa unafanyika ili kuweza kupata maelekezo sahihi.
Naye Mkuu wa Wilaya wa Songea Pololet Kamando Mgema alipewa nafasi ya kuzungumza katika Baraza hilo na kuwataka Madiwani kuendelea kuhamasisha wananchi juu ya kupata chanjo ya UVIKO 19 hata kwa kufanya mikutano ya hadhara katika maeneo yao.
IMEANDALIWA NA,
AMINA PILLY,
AFISA HABARI MANISPAA.
01.10.2021
SONGEA MUNICIPAL COUNCIL
Anuani ya Posta: P O BOX 14, SONGEA
Simu ya Mezani: 025 2602970
Simu ya Kiganjani:
Barua Pepe: info@songeamc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Manispaa ya Songea. Haki zote zimehifadhiwa