Mkoa wa Ruvuma ni miongoni mwa Mikoa ambayo ina sifa ya kuzalisha chakula kwa wingi nchini Tanzania, lakini pamoja na sifa hiyo bado kuna changamoto ya tatizo la utapiamlo na udumavu hasa kwa watoto wenye umri chini ya miaka mitano ambapo katika kupambambana na tatizo hilo kamati ya lishe ya Halmashauri ya Manispaa ya Songea imefanya kikao kazi kutathimini taarifa ya utekelezaji wa mkataba wa lishe kwa robo ya pili ya mwaka Oktoba hadi Disemba 2020, robo ya tatu kuanzia Januari hadi Machi 2021 pamoja na robo ya nne Aprili hadi Juni 2021,kikao kilichofanyika katika ukumbi wa Manispaa ya Songea leo tarehe 20 Agosti 2021 na kufunguliwa na Mkuu wa idara ya afya Manispaa ya Songea Dkt Amos Mwenda.
Akiwasilisha taarifa hiyo Afisa lishe Manispaa ya Songea Florentina Kissaka amebainisha jumla ya watoto 36748 wenye umri chini ya miaka mitano walifanyiwa uchunguzi wa hali ya lishe kwa kutumia mzingo wa mkono katika kipindi cha robo ya pili Oktoba hadi Disemba 2020 ambapo kati yao watoto 21 sawa na asilimia 0.1% waligundulika kuwa na utapiamlo mkali, watoto 434 sawa na asilimia 1.2% waligundulika kuwa na utapia mlo wa kadiri na watoto 36293 sawa na asilimia 98.7% hawakuwa na tatizo la utapia mlo “Alieleza”.
Kissaka aliongeza kuwa jumla ya akinamama wajawazito 9547 sawa na asilimia 98.2% walipatiwa nyongeza ya vidonge vya madini chuma/ asidi ya foliki katika kipindi chote cha ujauzito pia watoto 26,748 sawa na asilimia 99.9% wenye umri wa miezi 6 na kuendelea walipatiwa nyongeza ya vitamin A pamoja na kutoa elimu kwa akina mama wenye watoto chini ya miaka miwili juu ya namna ya uandaaji wa lishe bora na unasihi wa ulishaji wa watoto wachanga.
Kwa kipindi cha robo ya tatu Januari hadi Machi 2021 jumla ya watoto 37502 wenye umri chini ya miaka mitano walichunguzwa hali ya lishe na kati yao watoto 24 sawa na asilimia 0.2% waligundulika kuwa na utapiamlo mkali ambayo ni ongezeko la asilimia 0.1% ukilinganisha na robo ya pili iliyopita “Alibainisha”.
Katika kuendelea kupambana na udumavu pamoja na utapiamlo kwa kipindi cha robo ya nne Aprili hadi Juni kitengo kilifanya ukaguzi wa chumvi katika maduka na kuchukua sampuli za chumvi ili kuhakiki kiwango cha madini joto na baada ya uchunguzi sampuli 5 (10.2%) zilithibitika kuwa kiwango cha madini joto ya kutosha na sampuli 44 (89.8%) zilithibitika kutokuwa na kiwango cha madini joto ya kutosha ‘Kissaka alisema’.
Kamati imejipanga kuendelea kutoa elimu kwa wazazi kuhusu umuhimu wa chakula kwa wanafunzi wanapokuwa shuleni, kuhakikisha fedha za lishe kutoka idara mbalimbali zenye wanufaika zinatolewa kwa wakati, kutembelea kata zote 21 zilizopo ndani ya Manispaa ya Songea ili kutoa elimu juu ya matumizi sahihi ya viuatilifu na uzalishaji wa mazao mbalimbali hasa mbogamboga, mazao ya chakula sambamba na uhifadhi bora wa mazao hayo kwa wakulima kupitia mikutano mbalimbali ya hadhara .
IMEANDALIWA NA,
AMINA PILLY,
AFISA HABARI MANISPAA,
20.08.2021.
SONGEA MUNICIPAL COUNCIL
Anuani ya Posta: P O BOX 14, SONGEA
Simu ya Mezani: 025 2602970
Simu ya Kiganjani:
Barua Pepe: info@songeamc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Manispaa ya Songea. Haki zote zimehifadhiwa