HALMASHAURI ya Manispaa ya Songea mkoani Ruvuma imetoa mkopo wa shilingi milioni 70 kwa vikundi 46 vya wajasirimali wadogo.
Hafla ya kusaini mikataba ya mikopo hiyo imefanyika kwenye ukumbi wa SACCOS ya Halmashauri ya Manispaa ya Songea ambapo wajasiriamali hao wamepewa mafunzo ya namna ya kutumia mkopo huo.
Akitoa taarifa ya utoaji mikopo hiyo kwa vikundi vya wanawake,vijana na makundi maalum,Mkuu wa Idara ya Maendeleo ya Jamii katika Manispaa ya Songea NaftariSaiyoloi amesema kati ya fedha hizo,vikundi vya wanawake 26 vimekopeshwa zaidi ya milioni 29,vikundi 13 vya vijana vimekopeshwa zaidi ya shilingi milioni 27 na vikundi saba vya wenye ulemavu vimekopeshwa zaidi ya shilingi milioni 12.
Hata hivyo amesema katika fedha hizo,asilimia kumi ya mapato ya ndani ni zaidi ya shilingi milioni 120 na marejesho ni zaidi ya shilingi milioni 103 na kufanya jumla ya fedha zilizokopeshwa kuwa zaidi ya milioni 233 ambazo zimetolewa katika vikundi 143.
“Kuanzia mwaka huu wa fedha wa 2018/2019 hakutakuwa na riba ya asilimia 10 kama ilivyokuwa miaka ya nyuma,hivyo vikundi vyote vinakopeshwa na wanatakiwa kurejesha kiasi wanachokopeshwa’’,amesisitiza Saiyoloi.
Kulingana na Saiyoloi,katika kipindi cha mwaka 2018/2019 Manispaa ilifanikiwa kukopesha zaidi ya shilingi milioni 154 na kwamba fedha hizo ni kati ya lengo la kukopesha zaidi ya shilingi milioni 175.
Hata hivyo amesema katika kipindi hicho vikundi vya wanawake 52 vimekopeshwa zaidi ya shilingi milioni 62,vikundi vya vijan 32 vimekopeshwa zaidi ya shilingi 62 na vikundi vya wenye ulemavu 13 vimekopeshwa zaidi ya milioni 30 na kufanya vikundi 97 kukopeshwa.
Imeandaliwa na Albano Midelo
Afisa Habari Manispaa ya Songea
SONGEA MUNICIPAL COUNCIL
Anuani ya Posta: P O BOX 14, SONGEA
Simu ya Mezani: 025 2602970
Simu ya Kiganjani:
Barua Pepe: info@songeamc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Manispaa ya Songea. Haki zote zimehifadhiwa