WAZIRI Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Kassim M. Majaliwa (MB) ametoa rai kwa Madiwani, Wakurugenzi na Makatibu Tawala wa Mikoa kubadilisha mtazamo katika suala zima la usimamizi, ukusanyaji na utumiaji wa fedha zinazokusanywa kwenye Halmashauri zote nchini
Akifungua Mkutano Mkuu wa 34 wa Jumuiya ya Tawala za Mitaa Tanzania (ALAT) uliofanyika leo katika ukumbi wa Jakaya Mrisho Kikwete Jijini Dodoma. Mhe. Majaliwa amesema ustawi wa jamii unategemea uwezo wa mapato yake na matumizi yenye tija kwa fedha zinazokusanywa
Mhe. Majaliwa amefafanua kuwa lengo la Serikali ni kuhakikisha Halmashauri zinakuwa na uwezo wa kujitegemea kimapato kwa zaidi ya asilimia 80 ifikapo mwaka 2025 ili kutimiza lengo la Serikali katika Dira ya Maendeleo ya 2025.
Amesema kuwa Serikali ya awamu ya Tano imekuwa ikichukua hatua mbalimbali ili kuhakikisha dira ya maendeleo ya mwaka 2025 kwa kuanzisha utaratibu wa kugharamia miradi ya kimkakati yenye lengo la kuziongezea Halmashauri mapato ya uhakika na kupunguza utegemezi wa ruzuku ya Serikali.
Mhe. Majaliwa amesema kuwa hadi sasa Serikali imeidhinisha shilingi bilioni 131.5 kutekeleza miradi ya ipatayo 22 katika Halmashauri 17 zilizokidhi vigezo kwenye Mikoa 10 na mpaka sasa kiasi cha shilingi bilioni 16.4 zimepelekwa kwenye Halmasahauri hizo kwa ajili ya kuanza utekelezaji wa miradi ya kimkakati.
Amaesema kuwa uchambuzi wa miradi mingine ya kimaendeleo unaendelea na Halmashauri zitakazokidhi vigezo zitapata fedha kwa ajili ya utekelezaji wa miradi hiyo na amezitaka Halmashauri zote nchini kutumia fedha hizo kwa ajili ya malengo yaliyokusudiwa.
“ Serikali haitakuwa na utaratibu wa kutoa fedha bila kufahamu kwa kina fedha hizo zinakwenda kufanya nini na zinaleta mabadiliko gani kwa kuwa nimesikia kwamba katika baadhi ya Halmashauri fedha zilizokwishatolewa bado hazijaanza kutumika kikamilifu, nawaagiza Waheshimiwa Madiwani kusimamia matumizi ya fedha hizo ili Halmashauri zipate miradi yenye ubora unaotakiwa na inayokamilika kwa wakati” Anafafanua Majaliwa.
Mhe. Majaliwa amesema Serikali imeongeza ukusanyaji wa mapato katika Mamlaka za Serikali za Mitaa kwa kuhakikisha Halmashauri zote 185 zinatumia Mfumo wa ukusanyaji wa mapato wa Mamlaka za Serikali za Mitaa na kufanya ongezeko la mapato kutoka shilingi bilioni 379 kwa mwaka 2014/2015 hadi kufikia shilingi bilioni 553.39 kwa mwaka wa fedha 2017/2018 .
Amewaonya Viongozi wa Halmashauri wanaolalamikia kutokuendelea kulalamika kuhusu baadhi ya vyanzo vya mapato kuchukuliwa na Serikli kuu bali waongeze bidii na ubunifu katika kutafuta vyanzo vipya vya mapato ili Mamlaka za Serikali za Mitaa ziweze kujitegemea.
“Fanyeni kazi ionekane, tusione Mamlaka za Serikali za Mitaa ambazo kweli zinatoa huduma, tuone vyumba vya madarasa vinaongezeka, watoto hawakai chini, Zahanati zinazopendeza hapo tunaweza kusema sasa Halmashauri zimekomaa” Amefafanua Mhe. Majaliwa
Wakati huo huo Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa Mhe. Selemani Jafo amewaagiza Wakurungenzi wa Halmashauri kuacha kufanyakazi kwa mazoea bali wafanye kazi kwa bidii kwa kutumia weledi ili kuleta mabadiliko katika utendaji kazi katika Halmashauri
Aidha Mhe. Jafo amewaagiza Wakurugenzi wa Halmashauri zote nchini kuhakikisha wanatenga fedha kwa ajili ya kuwakopesha wanawake, vijana na watu wenye ulemavu ili kuwawezesha kiuchumi na kupunguza umaskini nchini.
Imetolewa na tovuti ya TAMISEMI
Septemba 27,2018
SONGEA MUNICIPAL COUNCIL
Anuani ya Posta: P O BOX 14, SONGEA
Simu ya Mezani: 025 2602970
Simu ya Kiganjani:
Barua Pepe: info@songeamc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Manispaa ya Songea. Haki zote zimehifadhiwa