HIFADHI ya Taifa ya Kitulo, ipo katika ukanda wa Nyanda za Juu Kusini mwa Tanzania, ikiwa katikati ya safu za milima ya Uporoto, Kipengule na Livingstone.
Sehemu kubwa ya hifadhi hii imetapakaa katika mikoa miwili ya Mbeya na Njombe. Eneo tengefu la hifadhi hii, limejumuisha safu za Kitulo na sehemu ya safu za milima ya Livingstone.
Hii ni hifadhi ya kwanza kabisa kutambulika katika ukanda wa Kitropiki katika Afrika, kuwahi kuanzishwa kwa minajili ya utunzaji wa mimea asilia ambayo sehemu kubwa ni maua.
Kutokana na kuwa eneo adimu duniani ambalo linavutia kutokana na muonekano wa maua,hifadhi imepewa majina mbalimbali kama bustani ya Afrika na wengine wameipa jina la Bustani ya Mungu.
Wazo la kuwepo kwa hifadhi hii, lilianzishwa na Asasi yenye kujihusisha na utunzaji wa wanyama na uoto asilia ya Wildlife Conservation Society (WCS), baada ya jopo la wataalamu kutoka asasi hii kuanza kuguswa na ukuaji wa biashara ya mimea asilia ambayo ipo katika hifadhi hii peke nchini.
Hifadhi ya Kitulo Mwaka 2005, ilitangazwa rasmi katika gazeti la serikali na kuwa ni miongoni mwa Hifadhi za Taifa nchini.
Hifadhi ya Taifa ya Kitulo, ina aina mbalimbali za mimea ipatayo 350, ambazo zimeshaandikishwa rasmi hadi sasa, ikiwa ni pamoja na aina 45 za mimea inayojulikana kitaalamu kwa jina la "Orchids", ambayo kimsingi haipatikani sehemu nyingine yoyote ile duniani.
Mwandishi wa Makala haya ni Albano Midelo
Afisa Habari Manispaa ya Songea
Simu 0784765917
SONGEA MUNICIPAL COUNCIL
Anuani ya Posta: P O BOX 14, SONGEA
Simu ya Mezani: 025 2602970
Simu ya Kiganjani:
Barua Pepe: info@songeamc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Manispaa ya Songea. Haki zote zimehifadhiwa