HIFADHI ya Taifa ya Serengeti inayopita katika mikoa ya Arusha,Mwanza,Mara na Shinyanga ni eneo pekee duniani lenye kundi kubwa la wanyama wanaohama katika mfumo mzima wa mlishano.
Inasemekena neno Serengeti linatokana na neno la kimasai la sirenget lenye maana ya uwanda mpana wa nyasi fupi,malisho mengi na maji ya kutosha pengine ndiyo maana hifadhi hiyo inapewa majina mengi kama vile lulu,bustani ya Afrika na Edeni ya Afrika kutokana na utajiri wa maliasili uliopo ndani ya hifadhi hii.
Hifadhi ya Taifa ya Serengeti yenye ukubwa wa kilometa za mraba 14,763 ilianzishwa mwaka 1951, ni Hifadhi ya Taifa ya pili kwa ukubwa nchini ikitanguliwa na hifadhi ya Taifa ya Ruaha yenye ukubwa wa kilometa za mraba 20,226.
Umaarufu wa hifadhi ya Taifa ya Serengeti unatokana na kuwa na misururu mirefu ya nyumbu wanaohama kwa makundi na kuvuka hata mpaka wa Tanzania hadi hifadhi ya wanyama pori ya Maasai Mara nchini Kenya ambapo takwimu za TANAPA zinaonesha kuwa kila mwaka zaidi ya nyumbu milioni moja,pundamilia 200,000, swala tomi zaidi ya 300,000 na pofu 12,000 huunga misafara ya kutafuta malisho na maji.
Mhifadhi John Makunga anasema Kila mwaka katikati ya mwezi Julai tukio lisilokuwa na kawaida na lenye mvuto wa kipekee hutokea katika hifadhi ya Taifa ya Serengeti kwa kundi kubwa la nyumbu wakikimbia kutoka upande wa kusini mwa hifadhi hiyo.
Hifadhi ya Taifa ya Serengeti huchukuliwa kama moja ya maajabu ya dunia kutokana na tendo la uhamaji wa nyumbu kutoka kusini hadi kaskazini na kurudi, tendo ambalo linafanyika mara moja tu kwa mwaka tendo hilo linaifanya hifadhi hii kuwa Eden ya Afrika na kupendwa kutembelewa na watu wengi ulimwenguni kote.
Makala imeandaliwa na Albano Midelo
Afisa Habari wa Manispaa ya Songea
SONGEA MUNICIPAL COUNCIL
Anuani ya Posta: P O BOX 14, SONGEA
Simu ya Mezani: 025 2602970
Simu ya Kiganjani:
Barua Pepe: info@songeamc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Manispaa ya Songea. Haki zote zimehifadhiwa