UGONJWA hatari wa homa ya nguruwe umeingia katika Manispaa ya Songea mkoani Ruvuma ambapo hadi sasa zaidi ya nguruwe 100 wamekufa.
Afisa Mifugo wa Halmashauri ya Manispaa ya Songea Rozina Chuwa amesema katika kipindi cha wiki mbili vimetokea vifo hivyo 100 vya nguruwe na kwamba hadi kufikia Jumapili iliyopita nguruwe 48 walikuwa wamekufa kutokana na ugonjwa huo.
Amesema ugonjwa huo unaonezwa virusi aina ya African Swine Fever Virus’ hauna kinga na unaenea kwa kasi kubwa katika Manispaa ya Songea yenye jumla ya nguruwe 4581 ambapo ametaja maeneo ambayo yanaongoza kuathirika na ugonjwa huo ni Lizaboni ambako nguruwe zaidi ya 100 wamekufa.
Maeneo mengine ambayo yameripotiwa kuingia ugonjwa huo Januari 24 na 25 mwaka huu ni Ruhuwiko, Mshangano na Mjimwema.
“Kwa kuwa ugonjwa wa homa ya nguruwe hauna kinga,kitaalam inashauriwa njia rahisi ya kukabiliana na ugonjwa huu ni kuchinja nguruwe ambao wapo katika maeneo ambayo umetokea ugonjwa huo ambao unaua nguruwe kwa kasi’’,anasisitiza Chuwa.
Hata hivyo amesema njia hiyo inakuwa ngumu kutekelezeka kwa sababu wananchi wengi hawakubali kuchinja nguruwe wao,hali ambayo inasababisha ugonjwa huo kuenea kutokana na kununua nyama ya nguruwe wenye ugonjwa.
Amesema ugonjwa huo haina madhara kwa binadamu ambapo kitaalam nguruwe aliyekufa kwa ugonjwa huo anatakiwa kuzikwa katika shimo lililopuliziwa dawa lenye urefu wa zaidi ya meta moja.
“Sisi kama wataalam wa Afya ili kudhibiti ugonjwa wa homa ya nguruwe tunashauri kuzuia kabisa biashara ya nyama ya nguruwe kwa sababu ugonjwa huu hauna kinga’’,anasisitiza Chuwa.
SONGEA MUNICIPAL COUNCIL
Anuani ya Posta: P O BOX 14, SONGEA
Simu ya Mezani: 025 2602970
Simu ya Kiganjani:
Barua Pepe: info@songeamc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Manispaa ya Songea. Haki zote zimehifadhiwa