Na,
AMINA PILLY,
AFISA HABARI MANISPAA.
23 MEI 2022
Mganga Mkuu wa Hospitali ya rufaa ya Mkoa wa Ruvuma Dkt. Magafu Majura amepokea vifaa tiba mtandao kutoka Wizara ya Afya leo tarehe 23 Mei 2022.
Akizungumza wakati wa kupokea vifaa hivyo Dkt Majura alisema, vifaa hivyo vitatumika katika eneo la kupiga X-ray na Utra sound (Radiology) ambapo vipimo vitakavyofanyika vitaunganishwa katika mtandao na kwenda moja kwa moja katika Hospitali za kanda na Taifa.
Ameeleza kuwa lengo la kutumia vifaa hivyo ni kurahisha gharama za matibabu kwa kutuma majibu ya vipimo vya mgonjwa husika kabla ya kusafirishwa na kuwawezesha madaktari bingwa waliopo Hospitali za kanda na Taifa kutatua changamoto ya ugonjwa husika kwa njia ya mtandao.
Dkt Majura ameishukuru Serikali ya Awamu ya sita kwa kuiwezesha Hospitali ya rufaa ya Mkoa wa Ruvuma kupata vifaa hivyo pamoja na kuleta fedha ambazo zimetumika katika ujenzi wa jengo la dharura pamoja na jengo la wagonjwa mahututi.
Mratibu wa huduma za tiba mtandao Wizara ya Afya Tanzania Dkt. Liggyle Vumilia amesema vifaa hivyo vimeletwa Mkoani Ruvuma kufuatia utekelezaji wa agizo la Waziri Mkuu Mhe. Kassimu Majaliwa alipofika katika Hospitali hiyo mnamo Januari 5, 2019 kwa lengo la kuzindua X-ray ya kidigitali ambapo aliagiza Hospitali hiyo iungwe na huduma ya tiba mtandao.
Aliongeza kuwa Hospitali ya rufaa ya Mkoa wa Ruvuma ni miongoni mwa hospitali nyingine nne zilizo pokea vifaa hivyo ikiwemo na hospitali za rufaa ya Mkoa wa Katavi,Tanga, hospitali za Wilaya ya Nzega na Chato ambapo vifaa vyote vimegharimu jumla ya Shilingi Billion 1 moja fedha ambazo zimetolewa na mfuko wa mawasiliano kwa wote (Universal communication Access Fund) kwa ajili ya ununuzi wa vifaa hivyo pamoja na gharama za uwekezaji.
Amebainisha kuwa jumla ya hospitali nyingine 16 za Mikoa zinatarajiwa kupelekewa vifaa hivyo kwa lengo la kuboresha utoaji wa huduma hasa kwa wananchi wanaoishi pembezoni kwa kupunguza gharama za kusafiri ili kupata huduma hizo.
Naye, Kaimu Mkuu wa kitengo cha mawasilino Serikalini Wizara ya Afya Catherine Sungura amesema kuwa Serikali ya Awamu ya 6 inaendelea kufanya maboresho katika sekta ya Afya nchini pamoja na kuhakikisha huduma za afya zinazotolewa kwa ubora na kwa wakati.
Amesema kuwa shilingi Million 630 zilitolewa na Serikali kwa ajili ya ujenzi wa jengo la kisasa la wagonjwa wa dharura pamoja na shilingi Million 150 ya ujenzi wa jengo la wagonjwa mahututi ambapo majengo yote ujenzi umekamilika kwa asilimia 100% na yataanza kutumika hivi karibuni.
Mwisho.
SONGEA MUNICIPAL COUNCIL
Anuani ya Posta: P O BOX 14, SONGEA
Simu ya Mezani: 025 2602970
Simu ya Kiganjani:
Barua Pepe: info@songeamc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Manispaa ya Songea. Haki zote zimehifadhiwa