SEKTA ya mafuta na gesi asilia ambayo iligundulika kwa mara ya kwanza hapa nchini mwaka 1974 katika kisiwa cha Songosongo mkoani Lindi,ugunduzi mwingine umefanyika Mkoa wa Mtwara mwaka 1982 eneo la Mnazibay,jumla ya gesi asilia iliyogundulika nchi kavu na baharini inafikia takriban futi za ujazo trilioni 55.08 hadi kufikia Machi 2015.
Mwandisi Mwandamizi kutoka Shirika la Maendeleo ya Petroli nchini TPDC Injinia Modestus Lumato anazitaja changamoto zilizopo katika sekta ya mafuta na gesi kuwa ni pamoja na gharama kubwa ya kuchimba visima wakati wa utafiti ambapo kisima kimoja kinaweza kugharimu sh.bilioni160.
Mafuta na gesi asilia yanaweza kupatikana katika miamba tabaka (sedimentary rocks) ndiyo yenye uwezo wa kutoa mafuta au gesi ambapo hapa Tanzania maeneo hayo ni ya pwani,Mtwara,na Lindi na mabonde ya nchi kavu.Utafiti unaonesha kuwa karibu nusu ya Tanzania kuna uwezekano wa kupatikana mafuta na gesi.
Utafutaji,uhakiki,uendelezaji na uzalishaji katika mafuta unaweza kuchukua miaka mitano wakati gesi inachukua muda mrefu zaidi kwa mfano gesi ya Songosongo iligundulika mwaka 1974 lakini uzalishaji umeanza mwaka 2004.
Changamoto zinazoikabili sekta ya mafuta na gesi ni upungufu wa watalaam,utafutaji kuwa kwenye makazi ya watu kama mafuta ya Kyela,kushindwa kufanyika utafiti kwenye hifadhi za Taifa,mgogoro wa mpaka baina ya nchi mbili kama ilivyo ziwa Nyasa kwa kuwa maumbile ya gesi na mafuta yanaweza kuvuka mipaka ya nchi.
Gesi asilia inatarajia kuanza kuzalishwa na kusafirishwa mwaka 2021.Hata hivyo Gesi asilia sio rasilimali ya kudumu ikianza kuvunwa inaweza kumalizika hivyo ni vema kuanzishwa mfuko wa mapato katika rasilimali ya gesi asilia na mafuta ili iwe na faida kwa kizazi cha sasa na kijacho
Rasilimali za madini,gesi na mafuta kadri zinavyoendelea kuchimbwa ndivyo zinazidi kupungua na hatimaye siku moja zitamalizika na kuacha ardhi ikiwa na mashimo hivyo ni vema serikali kuwa na sheria bora ya gesi asilia ambayo itazingatia kuwanufaisha watanzania wa leo na kesho.
Nchi inaweza kushindwa kunufaika na rasilimali hiyo,endapo usimamizi madhubuti hautafanyika kuanzia hatua za awali za kufanyika tathmini ya mazingira yaani Environmental Impact Assessment (EIA) ambayo ni muhimu kufanyika kabla ya mradi mkubwa kuanza hivyo wananchi wanatakiwa kushirishwa kikamilifu kuepusha athari za kimazingira endapo mradi unazidi faida au hasara.
Sheria mama ya ardhi inaelekeza EIA inatakiwa kufanyika katika hatua zote kwa kuwashirikisha wananchi na ripoti kuandikwa kwa lugha rahisi pia kuepuka kutoa makabulasha ambayo mwananchi wa kawaida anashindwa kusoma na kuelewa,mchakato mzima wa EIA ni lazima uzingatie kanuni na miongozo yote ili wananchi watambue manufaa watakayopata katika mradi huo pia kama mradi una madhara.
Changamoto nyingine zilizopo katika sekta gesi asilia na mafuta ni Shirika la Maendeleo ya Petroli nchini (TPDC) kuwa ni Taasisi dhaifu nchini ya kusimamia gesi na mafuta kwa kuwa haina mtaji na mikataba kwa mujibu wa sheria ya mafuta ya mwaka 1980,Waziri wa Nishati na Madini ndiye amepewa mamlaka ya kusaini mikataba yote na TPDC kazi yake ni kusimamia na kutoa leseni za utafutaji wa mafuta na gesi asilia.
Changamoto nyingine ni sheria ya madini ambayo inasema kuwa kampuni zote za utafutaji na uchimbaji zinapofika Tanzania kutoka nje zinatakiwa kuwa za kitanzania,lakini ukitokea mgogoro kampuni inakwenda kusuluhisha mgogoro nje ya nchi ikidai kuwa sio kampuni ya Tanzania.
Sheria ya madini ya mwaka 2010 inatoa mwanya wa kupokea rushwa kwa waziri husika kutoka kwa mwekezaji,nadhani TPDC ingepewa meno ya kufanyakazi moja kwa moja badala ya waziri.
Pesa ambazo zitokana na sekta ya gesi asilia na mafuta zinatakiwa kuwekwa katika mfuko maalum kama inavyofanyika katika nchi zilizofanikiwa kwenye sekta hiyo mfano Norway na Botswana ambazo zina mifuko huru ya fedha zinazotokana na sekta hizo.
Bila kuundwa kwa mifuko huru ya kusimamia mapato,ina maana kuwa fedha zinazopatikana katika sekta hizo endapo zote zitaingizwa katika matumizi zinaweza kuvuruga uchumi na baada ya miaka michache nchi inaweza kuwa na hali mbaya kiuchumi.
Mapato ya pesa itakayotokana na gesi asilia na mafuta inatakiwa kuingizwa kwenye uchumi kidogo kidogo ili kunufaisha kizazi cha sasa na kijacho kwa kuwa mwanzoni iwapo pesa zitatumika zote katika bajeti ya serikali nchi itaonekana inakwenda vizuri kiuchumi lakini miaka michache nchi itaanguka kiuchumi kwa kuwa rasilimali hizo zinakwisha.
Hata hivyo sekta ya madini,gesi asilia na mafuta ili iweze kuleta faida na maendeleo dumivu katika nchi ni lazima mfuko huo kuongozwa katika misingi ya ujuzi chini ya Bodi huru ambayo haitaingiliwa na wanasiasa mfano nchi ya Botswana ina mifuko huru mitano ambayo ina fedha za elimu,afya,huduma za jamii, barabara, mazingira na inafanya kazi bila kuingiliwa na wanasiasa au dola.
-ITAENDELEA--
Makala imeandikwa na Albano Midelo,mawasilino yake ni albano.midelo@gmail.com,simu 0784765917
SONGEA MUNICIPAL COUNCIL
Anuani ya Posta: P O BOX 14, SONGEA
Simu ya Mezani: 025 2602970
Simu ya Kiganjani:
Barua Pepe: info@songeamc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Manispaa ya Songea. Haki zote zimehifadhiwa