CHAMA cha akiba na mikopo SACCOS Manispaa ya Songea kilianzishwa januari 1988 na kuandikishwa rasmi Aprili 1988 kwa namba RVR 153 kikiwa na wanachama 20, lakini idadi hiyo imeendelea kuongezeka hadi sasa kufikia idadi ya wanachama 288 me 110 na ke 178 licha ya wanachama wengine kujiondoa kutokana na sababu ya kifo, kustaafu, kuhama, na matatizo ya kiuchumi.
Hayo yamebainika katika mkutano wa kawaida wa 28 wa chama cha akiba na mikopo SACCOS uliofanyika katika ukumbi wa St.Augustine uliopo Manispaa ya Songea leo tarehe 26.12.2020.
Mgeni rasmi katika Mkutano huo alikuwa Meneja wa Biashara na Mahusiano NMB tawi la Songea Augustino Manguya ambaye alianza kwa kutoa pongezi kwa viongozi wote ambao wamemaliza muda wao wa uongozi kwa muda wa miaka mitatu kwa uendeshaji mzuri wa chama.” Aliwapongeza.
Manguya aliwataka wanachama wote kukopa chamani sambmba na kuanzisha au kuboresha miradi yao ili kujiongezea kipato , pamoja nakufanya marejesho ya mikopo ili kuzidi kuimarisha chama na kuwa mkopaji bora kwa kufanya hivyo Chama kitaweza kukua kimtaji.
Naye Katibu wa chama cha SACCOS Winifrida Komba aliweka bayana masharti ya chama hicho ambayo yanasema “ kifungu cha 41(2) g, kinasema mkutano mkuu wa kawaida huthibitisha majina ya wanachama wapya na wanaojitoa na kuchukua hatua ya kinidhamu kwa baadhi ya wanachama wanaokiuka masharti ya chama ambapo katika mkutano huo walithibitsha wanachama wapya 27 na kuwaondoa wanachama 19 waliokoma uanachama kwasababu mbalimbali ikiwemo kifo, kustaafu, kuhama, na matatizo ya kiuchumi”
Naye mwenyekiti wa SACCOS Iddi Waziri ambaye amemaliza muda wake wa uongozi alisema mwaka 2019 chama kilikisia kukusanya shilingi 550,000,000/= hali halisi ya hadi disemba 2019 ilikusanywa shilingi 523,450,059.00 sawa na asilimia 95% ya lengo walilojiwekea sambamba na utoaji wa mikopo iliyotolewa kwa asilimia 93%.
Waziri alitanabaisha kuwa mwaka 2020 chama kiliweka makisio ya mapato shilingi 81,800,000/= kutokana na faida ya juu ya mkopo, viingilio, na mapato mengine na kuwa hali halisi ya makusanyo shilingi 80, 870, 785.15 sawa na asilimia 98.8 ya makisio hadi disemba 2020, ikiwa na mafanikio ya kukopesha wanachama 208 yenye thamani ya shilingi 458, 650, 000/= sawa na asilimia 109 ya lengo walilojiwekea.
Akitaja baadhi ya changamoto zinazoikabili chama hicho ni pamoja na baadhi ya wanachama waliopewa mkopo kutorejesha mikopo kwa wakati hali inayodhoofisha ufanisi wa chama na kuwa na mikopo chechefu isiyo na tija na kusababisha wanachama kushindwa kupatiwa mikopo kwa wakati, wanachama kukosa sifa ya kukopa kutokana baki ya moja ya tatu ya mshahara wake, baadhi ya marejesho ya mkononi kutorejeshwa kwa wakati, baadhi ya wanachama kukatwa chini ya kiwango, wanachama wanaochangia akiba kwa fedha tathilimu kushindwa kuchangia kwa wakati na nyinginezo.
Ufumbuzi wa changamoto hizo ni pamoja na wadaiwa sugu kesi zao kupelekwa TAKUKURU, wanachama wanaokatwa chini ya kiwango watoe ushirikiano ili kuweza kupewa taratibu za kuongezea marejesho yanayokatwa chini ya kiwango, wanachama wanaokosa moja ya tatu kuendelea kutumia utaratibu wa kutumia standing order ili waweze kuchangia chamani.
Alisema mnamo tarehe 09 julai 2020 bodi ilimsimamisha kazi Frola Luoga kwa makosa ya utovu wa nidhamu na kukosa uaminifu katika utendaji wake wa kazi na kuisababishia chama hasara ya kiasi cha fedha shilingi 4,847,101.75 pamoja na kushindwa kuwasilisha risiti ya makato ya watumishi NSSF kwa wakati na chini ya kiwango. Kutokana na kusimamishwa kwa kazi kwa Flora Luoga, chama kitatangaza nafasi hiyo kwa kufuata taratibu za ajira.
Mwisho alisema uchaguzi wa viongozi wapya ni sheria ya ushirika yamwaka 2015 ya kanuni za SACCOS 2018, ya masharti ya chama sehemu namba 48 na kifungu cha 4, inawaambia wanachama kuchagua viongozi bora wenye weredi watakaokiongoza chama kwa muda wa miaka mitatu ijayo.
Baada ya kusema hayo Afisa ushirika Given Mariki alitangaza matokeo ya uchaguzi wa wajumbe wa bodi pamoja Mwenyekiti na Makamu Mwenyekiti ambapo matokeo ya uchaguzi huo ndugu Amiri Ayuob alichaguliwa kuwa mwenyekiti aliyepita bila kupingwa, na makamu mwenyekiti Zacharia Kapinga alipata kura 158 dhidi ya mpinzani wake Bakari kawina aliyepata kura 26.
Mwisho mwenyekiti mteule Amiri Ayoub aliwashukuru wanachama kwakumchagua na kuomba ushirikiano kwa wanachama wote waliomchagua.
IMETYARISHWA NA;
AMINA PILLY;
AFISA HABARI MANISPAA YA SONGEA.
26 Disemba 2020.
SONGEA MUNICIPAL COUNCIL
Anuani ya Posta: P O BOX 14, SONGEA
Simu ya Mezani: 025 2602970
Simu ya Kiganjani:
Barua Pepe: info@songeamc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Manispaa ya Songea. Haki zote zimehifadhiwa