Na,
AMINA PILLY,
AFISA HABARI MANISPAA.
04.11.2021
Taasisi ya kuzuia na kupambana na rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Ruvuma imewataka viongozi waliopewa dhamana ya kusimamia fedha zilizotolewa na Serikali kuu kwa ajili ya mpango wa maendeleo kwa ustawi wa Taifa na mapambano dhidi ya UVIKO-19 kufuata miongozo sahihi ya matumizi ya fedha hizo.
Hayo yamebainishwa na Mkuu wa TAKUKURU Mkoani Ruvuma Hamza Mwenda alipozungumza na waandishi wa habari katika ofisi za makao makuu ya TAKUKURU Mkoani Ruvuma leo tarehe 4 Novemba 2021 kwa lengo la kutoa taarifa ya utekelezaji wa majukumu yake kwa kipindi cha robo ya kwanza ya mwaka wa fedha 2021/2022 iliyoanzia Julai – Septemba 2021.
Mwenda alisema kuwa viongozi wa Halmashauri husika Mkoani Ruvuma ambazo zimepokea fedha za utekelezaji wa miradi hiyo wanatakiwa kuhakikisha fedha hizo zinatumika kwa matumizi sahihi kwa kufuata muongozo uliotolewa na viongozi wa Serikali kuu.
Amewataka wananchi wote Mkoani Ruvuma kutoa ushirikiano kwa viongozi katika utekelezaji wa miradi iliyoainishwa kupitia mpango wa maendeleo kwa ustawi wa Taifa na mapambano dhidi ya UVIKO-19 pamoja nakuchukua hatua mahususi endapo wataona kuna viashiria vya ukiukwaji wa sheria za nchi na vitendo vya rushwa katika utekelezaji wa miradi husika.”Alisisistiza”
Katika kipindi cha miezi mitatu TAKUKURU Mkoani Ruvuma imefuatilia utekelezaji wa miradi ya maendeleo ya kumi na tatu yenye thamani ya shilingi bilioni moja na nusu (Tshs. 1,525,158,541/=) kwa lengo la kuhakikisha miradi hiyo inatekelezwa kwa kiwango kinachotakiwa na kwa kulinganisha na thamani ya fedha iliyotolewa ili kuzuia mianya ya rushwa na upotevu wa rasilimali katika utekelezaji wake.’Alieleza’
Miongoni mwa miradi iliyofatiliwa ni pamoja na mradi wa ujenzi wa vyumba viwili vya madarasa katika shule ya Msingi majimaji wenye thamani ya Tshs. 40,000,000/=, Mradi wa ujenzi wa vyumba viwili vya madarasa katika shule ya Sekondari Matemanga wenye thamani ya Tshs 40,000,000/=, mradi wa ujenzi wa vituo vya rasilimali za kilimo vya katika kata za Mbesa na Nakapanya wilayani Tunduru wenye thamani ya Tshs. 161,781,060/=, mradi wa ukarabati shule ya Sekondari Magazini wenye thamani ya Tshs. 30,000,000/= , mradi wa ujenzi wa chanzo na tenki la maji Likwilu wenye thamani ya Tshs 300,000,000/= wilaya ya Nyasa pamoja na miradi mingineyo. ‘Alibainisha’
Aliongeza kuwa kupitia kaguzi za miradi ambazo zilifanyika katika mbio maalum za mwenge wa uhuru zilizofanyika tarehe 2 – 6 mwezi Septemba 2021 katika Mkoa wa Ruvuma, miradi minne yenye thamani ya Tshs. 5,862,884,154.79 ilikataliwa na kukabidhiwa kwa TAKUKURU kwa lengo la kufanyiwa uchunguzi ambapo miradi hiyo ni pamoja na ujenzi wa Zahanati ya kijiji cha Uyahudini Wilaya ya Songea, mradi wa ujenzi wa madarasa, mradi wa maji safi kijiji cha Likuyu sekamaganga wilaya ya Namtumbo pamoja na ujenzi wa chuo cha ufundi VETA Wilaya ya Nyasa.
TAKUKURU Mkoa wa Ruvuma ilipokea jumla ya taarifa 74 za malalamiko juu ya matukio mbalimbali yanayohusiana na rushwa kutoka kwa wananchi kupitia vyanzo tofauti ambapo malalamiko hayo yote yalifanyiwa uchunguzi na kati ya malalamiko hayo ni malalamiko 52 yalihusishwa na rushwa ambayo tayari uchunguzi unaendelea.”Mwenda alisema”
Mwenda alibainisha vipaumbele vya TAKUKURU Mkoani Ruvuma katika kipindi cha Oktoba – Disemba 2021 ni pamoja na kufanya ufuatiliaji wa fedha zilizotolewa kwa ajili ya mpango wa maendeleo kwa ustawi wa Taifa na mapambano dhidi ya UVIKO-19, kuendelea na ufuatiliaji katika makusanyo ya fedha za ndani za Halmashauri kupitia utaratibu wa POS, Pamoja na kuendelea kutoa elimu kwa jamii kuhusiana na rushwa.
Mwisho.
SONGEA MUNICIPAL COUNCIL
Anuani ya Posta: P O BOX 14, SONGEA
Simu ya Mezani: 025 2602970
Simu ya Kiganjani:
Barua Pepe: info@songeamc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Manispaa ya Songea. Haki zote zimehifadhiwa