Kamati ya siasa Wilaya ya Songea Mjini imefanya ukaguzi na kuridhishwa na miradi mbalimbali ya maendeleo inayotekelezwa katika Halmashauri ya Manispaa ya Songea mkoani humo na kuupongeza uongozi wa Manispaa kwa kusimamia vyema miradi hiyo.
Kamati hiyo iliongozwa na mwenyekiti wa chama cha mapinduzi (CCM) mkoa wa Ruvuma Hamisi Abdalah Ally, sambamba na kamati ya siasa wilayani humo pamoja na viongozi wa serikali akiwemo na Mkuu wa Wilaya ya Songea Pololet Mgema ambapo ilitembelea miradi mitano tarehe 20 Agosti 2021 ambayo ni ujenzi wa choo katika shule ya sekondari Zimanimoto iliyopo kata ya Misufini, ujenzi wa bwalo la shule ya sekondari Emmanuel Nchimbi kata ya Msamala, ujenzi wa vyumba vya madarasa mawili, ukarabati wa madarasa matatu, ukarabati wa maabara pamoja na ujenzi wa matundu 12 ya choo katika shule ya sekondari Chandarua kata ya Mshangano, ujenzi wa madarasa 2, vyoo matundu 12 na samani katika shule ya msingi Ruhuwiko iliyopo kata ya Ruhuwiko pamoja na ukarabati wa miundombinu na samani katika shule ya msingi Juhudi iliyopo katika kata ya Ruvuma Manispaa ya Songea.
Akizungumza katika ziara hiyo mwenyekiti wa chama hicho mkoa wa Ruvuma amewapongeza viongozi wa wilaya ya Songea Mjini kwa kutekeleza vyema ilani ya chama cha mapinduzi kwani wanapokamilisha vyema miradi ya ujenzi wanakuwa wametimiza matakwa ya serikali ya chama cha mapinduzi.
Ameongeza kuwa si kwamba hakuna changamoto kabisa isipokuwa changamoto zilizopo kama vile uhaba wa maji katika maeneo ya miradi, kuchelewa kwa baadhi ya vifaa vya ujenzi pamoja na kuongezeka gharama za vifaa vya ujenzi ambazo zimeonekana katika baadhi ya miradi hiyo zinatakiwa kufanyiwa marekebisho ili kuweza kuharakisha kukamilishwa kwa miradi hiyo"Alieleza".
Pia amewataka viongozi wa serikali pamoja na kamati ya siasa ya wilaya kujenga mazoea ya kutembelea miradi mara kwa mara ili kuhakikisha ujenzi unafanyika kwa kiwango kinachotakiwa hali ambayo itasaidia kuepusha hasara ambayo inaweza kujitokeza na kuokoa muda kwani muda utakaotumika kubomoa na kujenga upya ingekuwa ni muda wa kutumia majengo.
Kwa upande wake Mstahiki Meya wa Manispaa ya Songea Michael Mbano ameahidi kuzifanyia kazi changamoto zote zilizoonekana ili kuweza kuyafanya miradi hiyo kukamilika kwa wakati na kwenye ubora unaotakiwa.
Miradi hiyo imetekelezwa kwa nguvu ya serikali ambapo ujenzi wa choo matundu saba katika shule ya sekondari Zimanimoto ulipokea shilingi milioni 7, ujenzi wa bwalo la shule ya sekondari Emmanuel Nchimbi ambao umegharimu shilingi ml.100, mradi wa ujenzi wa vyumba vya madarasa, vyoo na samani katika shule ya msingi Ruhuwiko ulipokea shilingi milioni 40, shule ya sekondari Chandarua ilipokea kiasi cha shilingi milioni 70 kwaaajili ya ujenzi wa madarasa na ukarabati wa maabara, ujenzi wa madarasa matatu na samani katika shule ya msingi Juhudi ambao umegharimu kiasi cha shilingi milioni 40.
NA AMINA PILLY,
AFISA HABARI MANISPAA,
24.08.2021.
SONGEA MUNICIPAL COUNCIL
Anuani ya Posta: P O BOX 14, SONGEA
Simu ya Mezani: 025 2602970
Simu ya Kiganjani:
Barua Pepe: info@songeamc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Manispaa ya Songea. Haki zote zimehifadhiwa