KAMATI ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya ya Songea ikiongozwa na Mwenyekiti wake Mkuu wa Wilaya ya Songea Pololet Mgema imekagua mradi wa machinjio ya kisasa unaotekelezwa katika Kata ya Tanga Manispaa ya Songea mkoani Ruvuma.
Akitoa taarifa ya mradi huo kwa Kamati hiyo kabla ya kuanza ukaguzi,Kaimu Mhandisi wa Ujenzi wa Manispaa ya Songea Mhandisi Nicolus Danda amesema mradi wa machinjio ya kisasa unafadhiliwa na Benki ya Dunia kwa gharama ya shilingi zaidi ya bilioni tatu.
Amemtaja Mkandarasi wa mradi huo ambaye hadi sasa amelipwa shilingi milioni 400 kuwa ni Kampuni ya Giraffe ambapo mkataba wake ni wa mwaka mmoja ambao umeanzia Julai 2017 na kukamilika Juni 30, 2018.
Kwa mujibu wa Danda kazi ambazo zinafanyika kwenye mradi huo ni ujenzi wa machinjio yenye urefu wa meta 64 na upana wa meta 24,ujenzi wa zizi lenye uwezo wa kuhifadhia ng’ombe 200 na ujenzi wa uzio,tanki la kuhifadhia maji lenye ujazo wa lita ya 162,000.
Kazi nyingine anazitaja kuwa ujenzi wa nyumba mbili ikiwemo ya daktari wa mifugo na mlinzi,ujenzi wa barabara ya kilometa moja ambayo itazunguka eneo la mradi na ujenzi wa maeneo ya kupaki magari.
Mkandarasi huyo ameahidi kumaliza kazi ndani ya mkataba ambapo amesema hivi sasa imebakia mistari michache kukamilisha kuzungusha jengo lote kisha kuanza kazi ya kjkamilisha maeneo yaliobakia pamoja na kuezeka machinjio.
Akizungumza mara baada ya ukaguzi wa mradi huo Mkuu wa wilaya ya Songea Pololet Mgema ameridhishwa na viwango vya ujenzi wa machinjio hiyo,hata hivyo ameshauri kuangaliwa upya viwango vya fedha ambazo zinatolewa kwa maoni yake anaona ni fedha nyingi ukilinganisha na kazi ambazo zinafanyika kwenye mradi husika.
Hata hivyo Mgema amempongeza Mkandarasi huyo kwa kazi kubwa ambayo ameifanya ukilinganisha na kiwango cha fedha cha shilingi milioni 400 ambazo ni malipo ya awali ambazo amelipwa hadi sasa na Manispaa ya Songea.
Wawakilishi toka Benki ya Dunia mwezi Machi mwaka huu wamefanya ukaguzi katika mradi huo na kuridhishwa na viwango vya ujenzi wa mradi huo.
Kamati ya Fedha na Uongozi ya Baraza la Madiwani la Manispaa ya Songea,tayari imekagua mradi huo na kuridhishwa na kazi ya Mkandarasi huyo.
Imetolewa na Albano Midelo
Afisa Habari Manispaa ya Songea
Aprili 6,2018
SONGEA MUNICIPAL COUNCIL
Anuani ya Posta: P O BOX 14, SONGEA
Simu ya Mezani: 025 2602970
Simu ya Kiganjani:
Barua Pepe: info@songeamc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Manispaa ya Songea. Haki zote zimehifadhiwa