TANZANIA imechaguliwa na Umoja wa Mataifa kuwa nchi ya kwanza kufanya kampeni ya kuhakikisha mwanamke anapata haki ya kumiliki ardhi kama ilivyo kwa wanaume.
Kampeni hii ni endelevu inafanyika kwa miaka 12 kuanzia mwaka 2019 hadi 2030 na inatarajiwa kuzinduliwa Novemba 21,2019 jijini Dar es salaam na Waziri wa Afya,Jinsia,Maendeleo ya Jamii,wazee na watoto Ummy Mwalimu.
Wadau 25 kutoka Taasisi mbalimbali wanashiriki katika kampeni hii likiwemo Shirika la kimataifa la Landesa ambalo ni Taasisi inayoshughulikia maendeleo vijijini na wanahabari ambao watasaidia kufanikisha kampeni hii kuwafikia watu wengi.
Godfrey Massay ni Mwanasheria na Mtaalam wa masuala ya ardhi kutoka Taasisi ya Landesi anasema Tanzania ina sera na sheria bora za ardhi ambazo zinakabiliwa na changamoto katika utekelezaji wake hivyo kusababisha baadhi ya watu kama wanawake kukosa haki za kumiliki ardhi .
“Tanzania imechaguliwa kuwa ya kwanza na Umoja wa mataifa kuona namna ya kuwasaidia wanawake kumiliki ardhi kwa sababu,ardhi ni maisha na kila kitu,sera na sheria nzuri zilizopo zinatakiwa zitekelezeke’’,anasisitiza Massay.
Hata hivyo anaitaja sababu ya Tanzania kuchaguliwa kuwa nchi ya kwanza kutekeleza kampeni hii kuwa ni kutokana na utashi wa serikali uliopo na kampeni zilizofanyika siku za nyuma kama Mama Ardhi kupata mafanikio makubwa.
Akizungumza wakati anatoa mafunzo maalum kwa wanahabari takribani 20 waliochaguliwa katika nchi nzima kujifunza habari zinazohusiana na haki ya mwanamke katika ardhi na uwekezaji wajibifu,Massay anasema mafunzo hayo yanatolewa kwa wanahabari kwa sababu wana namna nyingi za kufikisha ujumbe katika jamii.
Anasisitiza kuwa wakati sasa umefika duniani kote kuhakikisha mwanamke anapata haki ya kumiliki ardhi na kwamba hapa Tanzania kuanzia Katiba ya nchi ya mwaka 1977 hadi sheria ya ardhi ya mwaka 1999 kifungu cha nne na tano vinampa nafasi mwanamke kumiliki ardhi.
Imeandikwa na Albano Midelo,Songea
SONGEA MUNICIPAL COUNCIL
Anuani ya Posta: P O BOX 14, SONGEA
Simu ya Mezani: 025 2602970
Simu ya Kiganjani:
Barua Pepe: info@songeamc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Manispaa ya Songea. Haki zote zimehifadhiwa