MKOA WA RUVUMA WAFANIKIWA KUPUNGUZA KASI YA KUENEA MAGONJWA YALIYOKUWA HAYAPEWI KIPAUMBELE
Mkoa wa Ruvuma umefanikiwa kupunguza kiwango cha maambukizi ya magonjwa yaliyokuwa hayapewi kipaumbele kutokana na mwitikio mzuri wa jamii kutumia dawakinga.
Mafanikio haya yameelezwa leo(Jumamosi) na Mkuu wa mkoa wa Ruvuma Christina Mndeme wakati akifungua semina ya uraghibishi na uhamashishaji waa viongozi wa mkoa na Halmashauri mjini Songea kuhusu kuweka mkakati wa kuyakabili magonjwa yaliyokuwa hayapewi kipaumbele.
Amesema mkoa wa Ruvuma umekuwa ukikabiliana na magonjwa matano yaliyokuwa hayapewi kipaumbele ambayo ni Minyoo tumbo,Kichocho,Trakoma ,Usubi,Matende na Mabusha (Ngirimaji) katika Wilaya zote.
“Taarifa za Wizara ya Afya zinaonyesha kuwa mkoa wetu wa Ruvuma umeweza kupunguza kiwango cha maambukizi kwa magonjwa ya Trakoma,Matende na Mabusha “ alisema Mndeme
Mkuu wa Mkoa Mndeme amewapongeza Wananchi kwa kuitikia wito wa kumeza dawa kupitia kampeni mbalimbali zilizoratibiwa tangu mwaka 1998 serikali ilipoanzisha kampeni ya kudhibiti magonjwa yaliyokuwa hayapewi kipaumbele.
Akitoa mada Afisa Mpango Magonjwa Yaliyokuwa Hayapewi Kipaumbele Bw.Oscar Kaitaba amesema sababu za kusitisha utoaji dawa za Trakoma ,matende na Mabusha kwenye Halmashauri za Wilaya ya Songea,Namtumbo na Tunduru ni kutokana utafiti kuonyesha maambukizi kuwa chini ya asilimia moja.
Kuhusu ugonjwa wa Usubi ,Afisa Mpango Magonjwa Yaliyokuwa Hayapewi Kipaumbele toka Wizara ya Afya Bw.Oscar Kaitaba amesema mkoa wa Ruvuma unafanya vizuri katika kutokomeza ugonjwa huu na hasa Wilaya ya Tunduru.
“Taarifa nilizonazo nazo ni kwamba Wilaya hiyo inasubiri maelekezo ya Shirika la Afya Duniani ili waweze kusitisha unywesheshaji wa dawa za kutokomeza ugonjwa wa usubi.” Alisema Kaitaba
Kwa upande wake Mratibu wa Mkoa wa Magonjwa yaliyokuwa hayapwei kipaumbele Dkt,Charles Hinju ametoa takwimu za mkoa zinazonyesha kuwa mwaka 2016 jumla ya watu 1,052,907 kati ya 1,420,317 walipata kingatiba sawa na asilimia 74 huku kwa mwaka 2017 watu 1,192,390 kati ya 1,413,751 walipata kingatiba sawa na asilimia 84.
Uwepo wa magonjwa yasiyopewa kipaumbele katika mkoa wa Ruvuma umekuwa na madhara mengi kama kusababisha ulemavu,upofu wa kudumu,kupunguza rasilimali fedha kwa mahitaji ya dawa na unyanyapaa kwa wagonjwa
Imetolewa na
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Ruvuma
Songea
14 Octoba,2018
SONGEA MUNICIPAL COUNCIL
Anuani ya Posta: P O BOX 14, SONGEA
Simu ya Mezani: 025 2602970
Simu ya Kiganjani:
Barua Pepe: info@songeamc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Manispaa ya Songea. Haki zote zimehifadhiwa