HALMASHAURI ya Manispaa ya Songea mkoani Ruvuma imekuwa ikitekeleza shughuli za Mfuko wa wa Afya ya jamii (CHF) tangu mwaka 2006 ambapo shughuli za kuhamasisha jamii kujiunga na CHF zimefanyika katika kata zote 21.
Kaimu Mganga Mkuu wa Manispaa ya Songea Dk.Mameritha Basike amesema hadi kufikia machi 2018, kaya 7045 sawa na asilimia 16 zilikuwa zimejiunga na Mfuko wa Afya ya Jamii (CHF).
Dk.Basike amebainisha kuwa utoaji wa vitambulisho bure kwa wazee wenye umri wa kuanzia miaka 60 umefanyika kwa wazee 1,200 sawa na asilimia 10.9
“Kata tisa ambazo ambazo wazee wamenukaifa na vitambulisho hivyo ni Mjini, Misufini, Majengo, Bombambili, Matogoro, Lizaboni, Matarawe, Mateka na Seedfarm lengo likiwa ni kuwafikia wazee 11,678 katika Kata zote 21’’,anasisitiza.
Hata hivyo amesema wazee wote ambao hawajafikiwa na kupatiwa vitambulisho maalumu vya matibabu, watatambuliwa kwa vitambulisho vya kupigia kura.
Amesema Halmashauri imeingia mkataba na vituo vya kutolea huduma za afya ambavyo vinamilikiwa na Mashirika ya dini ili kutoa mitibabu bure kwa wazee 600 waliopo katika Manispaa hiyo.
Anazitaja changamoto za Mfuko wa Afya ya jamii kuwa ni ya kukosekana kwa vituo vya serikali vya kutolea huduma za afya kwa baadhi ya maeneo na sehemu nyingine vipo vituo vya taasisi za dini ambavyo kwa taratibu zao hawapokei au hawatoi huduma hiyo hali ambayo inachangia ugumu wa kuhamasisha jamii kujiunga na mfuko wa Afya ya jamii.
Hata hivyo Halmashauri inaendelea kufanyia kazi changamoto hiyo ili kuwezesha vituo vya Dini kutoa huduma hiyo kwa ufasaha na kuhamasisha Wananchi kuanzisha ujenzi kwa maeneo ambayo vituo vya Serikali vipo mbali na mitaa yao. Kulingana na takwimu za wazee za mwaka 2016,Manispaa ya Songea ina zaidi ya wazee 11,000.
Imeandaliwa na Albano Midelo
Afisa Habari Manipaa ya Songea
Mei 11,2018
SONGEA MUNICIPAL COUNCIL
Anuani ya Posta: P O BOX 14, SONGEA
Simu ya Mezani: 025 2602970
Simu ya Kiganjani:
Barua Pepe: info@songeamc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Manispaa ya Songea. Haki zote zimehifadhiwa