WANUFAIKA wapatao 4881 waliopo katika mpango wa kunusuru kaya masikini(TASAF) katika Halmashauri ya Manispaa ya Songea mkoani Ruvuma wamelipwa zaidi ya sh.milioni 175 katika kipindi cha Septemba na Oktoba 2017.Mratibu wa TASAF katika Manispaa ya Songea Christopher Ngonyani amesema malipo hayo yamefanyika na kukamilika wiki hii katika mitaa 53 yenye wanufaika wa TASAF katika Manispaa hiyo.
Hata hivyo amebainisha kuwa kati ya fedha hizo zaidi ya milioni 133 wamelipwa wanufaika 3608 kwa njia ya fedha taslimu ambapo zaidi ya milioni 42 wamelipwa wanufaika 1273 kwa njia ya mitandao ya simu.Amesema lengo ni kuhakikisha kuwa wanufaika wote wa TASAF wanaingizwa kwenye mfumo wa malipo kwa njia ya mtandao kwa kuwa malipo yanalipwa moja kwa moja na TASAF toka makao makuu badala ya fedha kutumwa katika Halmashauri hivyo kutumia muda mrefu hadi kuwafikia walengwa.
Utafiti uliofanywa katika mitaa mbalimbali ambayo wanufaika wamelipwa kwa njia ya mtandao,umebaini kuwa mfumo huo umepata mafanikio makubwa baada ya wanufaika wengi kupata fedha zao,ingawa changamoto ilijitokeza kwa baadhi ya kampuni za simu kushindwa kuwalipa wanufaika kwa njia ya mtandao.Manispaa ya Songea ni moja kati ya Halmashauri 16 nchini zilizochaguliwa kufanya majaribio ya malipo kwa mtandao wa simu kwa wanufaika wa TASAF ili kuepukana na changamoto zilizokuwa zimejitokeza za kutumia mfumo wa kulipwa fedha tasilimu.
Mpango wa kunusuru kaya masikini TASAF unaendeshwa katika Halmashauri 163 katika nchi nzima.Mpango huu umezinufaisha kaya masikini zikiwemo zile ambazo awali zilikuwa zinapata mlo mmoja kwa siku ambapo hivi sasa zinapata milo mitatu kwa siku.
Imetolewa na Albano Midelo
Afisa Habari Manispaa ya Songea
SONGEA MUNICIPAL COUNCIL
Anuani ya Posta: P O BOX 14, SONGEA
Simu ya Mezani: 025 2602970
Simu ya Kiganjani:
Barua Pepe: info@songeamc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Manispaa ya Songea. Haki zote zimehifadhiwa