KIJIJI cha Mpepo kipo katika Kata ya Mpepo Halmashauri ya wilaya ya Nyasa mkoani Ruvuma,kilianzishwa mwaka 1967 hadi sasa kina wakazi 3840.
Kata ya Mpepo yenye wakazi 8,978 inaundwa na vijiji vitano ambavyo ni Mpepo,Mindu,Kihuninga,Mtetema na Darpori.
Katika hali inayowashangaza wengi katika kijiji cha Mpepo hakuna tishio la ugonjwa wa malaria kama ilivyo katika vijiji,wilaya na mikoa mingi hapa nchini ambapo takwimu za kitaifa zinaonesha ugonjwa wa malaria unaoongoza kwa kusababisha vifo vingi.
Mwenyekiti wa Kijiji cha Mpepo Kilian Kumburu amesema unaweza kuishi katika kijiji hicho kati ya miaka 10 hadi 15 bila kupata ugonjwa wa malaria na kwamba baadhi ya watu hawaugui kabisa.
Hata hivyo bado haijulikani kwanini maambukizo ya vimelea vya malaria katika kijiji hicho yapo chini licha ya kuwepo mabonde yenye vyanzo vya maji,miti,nyasi na zao la kahawa.
Kulingana na Mwenyekiti huyo,asili ya neno Mpepo linatokana na kijiji hicho kuwa na upepo mkali kipindi chote cha mwaka unavuma toka ziwa Nyasa.Hata hivyo anasema upepo unavuma zaidi na kuezua nyumba na kuangusha miti katika kipindi cha kuanzia mwezi Januari hadi Februari.
Ili kukabiliana na upepo mkali wakazi wa kijiji hicho wanajenga nyumba fupi, ambazo zinaezekwa bati kwa kufungwa nondo ili kukabiliana na upepo mkali ambao umesababisha miti kupinda.
Imetolewa na Albano Midelo
Afisa Habari Ruvuma
SONGEA MUNICIPAL COUNCIL
Anuani ya Posta: P O BOX 14, SONGEA
Simu ya Mezani: 025 2602970
Simu ya Kiganjani:
Barua Pepe: info@songeamc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Manispaa ya Songea. Haki zote zimehifadhiwa