NA,
AMINA PILLY,
AFISA HABARI MANISPAA.
13.10.2021
Waziri wa Kilimo nchini Tanzania Profesa Adolf Mkenda ameongoza mamia ya Wananchi mkoani Ruvuma katika kuadhimisha siku ya mbolea duniani iliyofanyika leo tarehe 13 Oktoba 2021 katika uwanja wa Majimaji.
Mkenda alianza kwa kuwapongeza wakulima wa Mkoa wa Ruvuma kwa kuwa kitovu cha uzalishaji wa mazao ya chakula nchini hasa zao la mahindi kwa wingi na kuchangia kwa asilimia kubwa upatikanaji wa chakula kwa wananchi wa Tanzania.
Aliongeza kuwa ni muhimu kutumia siku hii ya mbolea duniani katika kuhimiza matumizi bora na sahihi ya mbolea ili kuleta tija katika maendeleo ya kilimo nchini lakini pia kwa wakulima wenyewe, hii ni kutokana na changamoto ya tija ndogo katika uzalishaji wa mazao ambapo sekta ya kilimo inachangia asilimia 15% tu katika pato la Taifa.”Alibainisha”
“Moja ya hatua sahihi ya kuongeza tija katika sekta ya kilimo ni kuhimiza matumiza sahihi ya mbolea kwa kiwango cha kutosha katika uzalishaji wa mazao yote ya chakula na biashara” Alisisitiza.
Aliendelea kwa kusema kuwa changamoto kubwa iliyopo sasa kwa wakulima ni kupanda kwa bei ya mbolea duniani na Tanzania kwa ujumla ambapo bei ya mbolea ya kuoteshea (DAP) kwa mfuko wa Kilogram 50 ni Tsh. 100000/= ukilinganisha na bei ya mwaka jana 2020 ambapo ilikuwa ni Tshs 48000/= hadi Tshs 65000/= katika maeneo tofauti nchini.
Mkenda alieleza sababu ya kupanda kwa bei ya mbolea duniani ni kutokana na janga la ugonjwa wa UVIKO 19 katika kipindi cha mwaka 2020/2021 hali iliyosababisha kupungua kwa uzalishaji wa mbolea viwandani na kusababisha ongezeko la uhitaji wa pembejeo hiyo pamoja na ongezeko la bei duniani kote ambapo hadi sasa matumaini ya kushuka kwa bei hizo bado hayajaonekana.
Hata hivyo Serikali imeamua kuchukua hatua mbalimbali ili kuhakikisha inapunguza makali ya upatikanaji wa mbolea kwa wakulima nchini kwa kufuta utaratibu wa kuagiza mbolea kutoka nje ya nchi kwa kutumia wazabuni na hivyo kutoa fursa kwa kila mfanyabiashara mwenye uwezo wa kuagiza mbolea bora na kuzileta nchini ili kusaidia ongezeko la upatikanaji wa mbolea kwa wingi. “Alieleza”
Ametoa wito kwa kampuni zote za mbolea nchini kuwaagiza mawakala wao kuhakikisha hawaongezi gharama za bei ya mbolea ili kujitengenezea faida kubwa badala yake waweke gharama nafuu ili kumsaidia mkulima kununua pembejeo hiyo.
Siku ya mbolea duniani huadhimishwa kila mwaka tarehe 13 Oktoba ikiwa ni kumbukizi ya uvumbuzi wa kirutubishi aina ya Amonia kinachopatikana hewani uliofanywa na mwana sayansi kutoka nchini Uingereza Fritz Haber mwaka 1908, na iliadhimishwa kwa mara ya kwanza duniani tarehe 13 Oktoba 2016 nchini Uingereza kwa lengo la kuelimisha umma kuhusu faida na matumizi sahihi ya mbolea.
Kauli mbiu katika maadhimisho hayo ni; “TUMIA MBOLEA BORA KWA TIJA NA KILIMO ENDELEVU”
Mwisho.
SONGEA MUNICIPAL COUNCIL
Anuani ya Posta: P O BOX 14, SONGEA
Simu ya Mezani: 025 2602970
Simu ya Kiganjani:
Barua Pepe: info@songeamc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Manispaa ya Songea. Haki zote zimehifadhiwa