KIONGOZI wa Mbio za Mwenge wa Uhuru 2018 Charles Kabeho amegawa vyandarua kwa wenye ulemavu wa viungo wapatao 20 wa kata ya Mshangano, wakiwa ni wawakilishi wa wenye ulemavu wenzao 600 wa kata 20 za Manispaa ya Songea mkoani Ruvuma.
Ugonjwa wa malaria ni miongoni mwa magonjwa 10 yanayowasumbua watu wengi katika Manispaa ya Songea,hususani akina mama wajawazito, na watoto chini ya miaka mitano.Mwaka 2017 Manispaa ya Songea ilikuwa na wagonjwa wa malaria waliopata matibabu ya nje 48,252 ambao ni sawa na asilimia 19 ya wagonjwa wote 250,038 waliopata matibabu ya nje. Wagonjwa waliougua ugonjwa na Malaria na kulazwa walikuwa 3,890 sawa na asilimia 12.8 ya wagonjwa wote 30,193 waliolazwa.
Watoto chini ya umri wa miaka mitano waliougua ugonjwa wa Malaria na kutibiwa matibabu ya nje walikuwa 17,231 sawa na asilimia 19 ya wagonjwa wote 89,861 chini ya miaka mitano. Watoto 1,586 waliolazwa kutokana na ugonjwa wa Malaria ni sawa na asilimia 24.3 ya watoto 6,520 waliolazwa kutokana na magonjwa mengine yote.
Aidha vifo vilivyotokea dhidi ya ugonjwa wa Malaria kwa mwaka 2017 ni 99 sawa na asilimia 29 ya vifo vyote 341 vilivyotokea kutokana na magonjwa mengine. Watoto chini ya miaka mitano waliokufa kutokana na ugonjwa wa Malaria ni 43 sawa na asilimia 18 ya vifo vyote vilivyotokea kwa watoto chini ya umri wa miaka mitano ambao ni 244.
Katika kuendeleza mapambano dhidi ya ugonjwa wa malaria, Manispaa imejiwekea mikakati ifuatayo;Kushirikiana na Serikali kuu kuendesha zoezi la mpango wa ugawaji vyandarua shuleni, kwa kina mama wajawazito na watoto wanaopata chanjo ya surua umri wa miezi tisa. kuendelea kununua dawa na vipimo vya Malaria (MRDT). Utoaji wa Elimu kuhusu kutumia vyandarua, kupima kabla ya kutibiwa, kuwahi matibabu mara unapoona dalili za malaria, kuwahi kliniki kwa mama mjazito na kuweka mazingira katika hali ya usafi.
Halmashauri ya Manispaa ya Songea inatekeleza mpango wa kuua viluwiluwi vya mbu kwenye mazalia. Kwa mwaka 2017 Halmashauri ilipokea dawa jumla ya lita 1,000 kutoka Serikali kuu ambayo imepuliziwa kwenye mazalia ya wazi, madimbwi mita za mraba 32,000 na mazalia yaliyofunikwa mita za ujazo 50,000. Mpango huu ni endelevu katika manispaa ya Songea.
Imetolewa na Albano Midelo
Afisa Habari Manispaa ya Songea
Juni 11,2018
SONGEA MUNICIPAL COUNCIL
Anuani ya Posta: P O BOX 14, SONGEA
Simu ya Mezani: 025 2602970
Simu ya Kiganjani:
Barua Pepe: info@songeamc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Manispaa ya Songea. Haki zote zimehifadhiwa