UFUGAJI wa samaki katika mabwawa ni moja ya shughuli inayopewa kipaumbele kwa jamii Mkoani Ruvuma, kwa kuwa shughuli hii inaongeza kipato, lishe na ajira kwa wananchi.
Kituo cha mabwawa ya ufugaji samaki na utalii wa ndani Luhira Kata ya Mshangano Manispaa ya Songea mkoani Ruvuma, kilianzishwa mwaka 1953 wakati wa Utawala wa Ukoloni wa Mwingereza.
Kwa mujibu wa Mkuu wa Kituo hicho Noel Kapinga,Kituo hicho kilikuwa chini ya mkoloni hadi nchi ilipopata uhuru kituo kikawa chini ya Wizara ya Maliasili na Utalii.
Hata hivyo Kapinga anasema Mwaka 2007 kituo kilikuwa kinamilikiwa na kikundi cha SOFFA kwa mkataba wa miaka mitano.
Mwaka 2008 Wizara ya Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi kupitia Idara yake ya Ukuzaji Viumbe kwenye Maji, iliingia mkataba na Halmashauri ya Songea pamoja na SOFFA ili izalishe vifaranga bora vya samaki na kutoa huduma za ugani kwa Kanda ya Nyanda za Juu Kusini Ili kukabiliana na changamoto ya upatikanaji wa mbegu bora ya samaki.
Kulingana na Kapinga Kituo hicho kina eneo lenye ukubwa wa ekari 68.45 sawa na hekta 28.5. Idadi ya mabwawa ni 13 yenye jumla ya mita za mraba 29,279 sawa na hekta 2.9. ambapo Mabwawa yanayotumika hadi sasa ni 13.
Hata hivyo anasema Kuanzia mwaka wa 2008 hadi 2018, Serikali kupitia Idara ya Ukuzaji Viumbe kwenye Maji chini ya Wizara ya Mifugo na Uvuvi, iliweza kutenga fedha za maendeleo kiasi cha Zaidi ya shilingi milioni 71 ambazo zililetwa kwa nyakati tofauti kwa ajili ya kuboresha mazingira ya uzalishaji kwa kuchimba, kujenga na kukarabati mabwawa 13, ukarabati wa stoo, darasa dogo la wafugaji na ujenzi wa kibanda cha Utalii.
Kapinga anayataja mafanikio ambayo kituo hicho kimeyapata kuanzia mwaka 2012 hadi Juni 2018,kuwa ni pamoja na Kituo kimezalisha jumla vifaranga vya samaki aina ya perege 452,767 ambapo jumla ya vifaranga 208,670 vyenye thamani ya shilingi 10,483,500/= vimesambazwa kwa wafugaji ndani na nje ya Mkoa wa Ruvuma.
Mafanikio mengine anayataja kuwa ni Kituo kimefanikiwa kutoa elimu kwa wafugaji zaidi ya 956 na vikundi 65 ndani na nje ya Mkoa wa Ruvuma na kituo cha Ruhila kimepata bahati ya kutembelewa na viongozi wa Kimkoa na Kitaifa ambapo mwaka 2013 Waziri Mkuu Mstaafu, Mizengo Kayanza Pinda.
“Kituo kilipokea ugeni wa mabalozi toka nchi za Msumbiji, Malawi na Zambia waliofika kushuhudia shughuli za uzalishaji wa samaki kwenye mabwawa zinazofanyika Mkoani Ruvuma’’,anasema Kapinga.
Anabainisha Zaidi kuwa kila mwaka kituo hicho kimekuwa kikipokea wastani wa wanafunzi wanne kutoka katika vyuo vya uvuvi wanaofika kujifunza kwa vitendo ambapo Zaidi ya wanafunzi 200 wamefika kati yao wanafunzi 20 wa shule za sekondari na wanafunzi 200 kutoka katika Chuo cha Mifugo LITA, MADABA.
Amesema Kituo hicho kimeendelea kushirikiana na taasisi mbalimbali nchini kama vile TAFIRI, SUA na UDSM ambapo shughuli mbalimbali za kitafiti zimefanyika kituoni ili kuleta tija katika uzalishaji wa samaki.
Anayataja matarajio ya baadaye ya kituo hicho kuwa ni kuendeleza ufugaji wa samaki katika mabwawa ya asili/malambo,Kuzalisha vifaranga bora vya samaki zaidi ya 4,200,000 kwa mwaka ili kuweza kukuza mahitaji katika kuendeleza ufugaji wa samaki kwenye mwabwawa ya asili na malambo.
Matarajio mengine ni Kutanua miundo mbinu ya uzalishaji wa mbegu ikiwa ni pamoja na utengenezaji wa ‘concrete tank’ na maabara ndogo ya upimaji wa maji na magonjwa ya samaki,majengo Rasmi ya ofisi za Kituo na Kuweka uzio eneo la kituo.
Hata hivyo Katika kutekeleza malengo na dira ya kituo,anazitaja changamoto mbali mbali ambazo zinakikabili kituo hicho kuwa ni ukosefu wa miundo mbinu ya kisasa ya uzalishaji wa vifaranga vya samaki,ukosefu wa usafiri wa uhakika kwa lengo la kurahisisha shughuli za ugani na kusafirishia vifaranga na kosefu wa hosteli.
Changamoto nyingine ni ukosefu wa ofisi ya kudumu,ukosefu wa umeme wa uhakika wa TANESCO,upungufu wa vitendea kazi/mashine ya kutengenezea chakula cha samaki na ukosekana kwa uzio wa kudumu kuzunguka eneo la kituo hicho.
Imetolewa na Albano Midelo
Afisa Habari Manispaa ya Songea
Juni 14,2018
SONGEA MUNICIPAL COUNCIL
Anuani ya Posta: P O BOX 14, SONGEA
Simu ya Mezani: 025 2602970
Simu ya Kiganjani:
Barua Pepe: info@songeamc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Manispaa ya Songea. Haki zote zimehifadhiwa