KUELEKEA maadhimisho ya siku ya mazingira duniani ambayo yanaanzia Mei 30 na kilele chake Juni 5 kila mwaka,uchafuzi wa mto Ruvuma unaofanywa na wachimbaji wa madini katika nchi ya Tanzania na Msumbiji unatishia ustawi wa viumbehai wakiwemo binadamu na viumbehai wa majini na ardhini.
Afisa Maliasili wa Mkoa wa Ruvuma Afrikanus Challe anasema wachimbaji wadogo wa madini ya dhahabu wanatumia mito inayomwaga maji yake mto Ruvuma kusafishia dhahabu kwa kutumia kemikali ya zebaki ambayo inaingia moja kwa moja hadi mto Ruvuma.Anaitaja mito midogo inayomwaga maji yake mto Ruvuma ambayo inaongoza kwa uchafuzi kuwa ni mto Lunyere na Lumeme kwa upande wa Tanzania na mito ya Msinje na Kipingi ambayo inaanzia nchini Msumbiji.
Challe anasema machimbo ya dhahabu katika maeneo ya Kizito,Mpepo,Ndondo,Luporo,Liumbe na Manyigu katika nchi za Tanzania na Msumbiji yapo kwenye vyanzo vya maji vya mito hiyo ambayo inamwaga maji yake katika mto Ruvuma ambao unamwaga maji yake Bahari ya Hindi.
“Wachimbaji toka nchi zote mbili wanafanya shughuli zao za uchimbaji bila tahadhari na kufuata kanuni na sheria za uchimbaji matokeo yake wanafanya uchafuzi ulisababisha mto Ruvuma kuathirika kwa kiwango kikubwa na kemikali za zebaki’ na takataka nyingine’,anasisitiza Challe.
Challe anashauri shughuli zote za uchimbaji jirani na vyanzo vya maji zinatakiwa kuzuiwa na nchi zote mbili kwa kuwa vipimo vya maabara vinaonesha kuwa mto Ruvuma una kiwango kikubwa cha zebaki ambacho kinaweza kuathiri binadamu na viumbehai.
Kwa mujibu wa matokeo ya maabara kwenye vyanzo vya maji vya Songeapori mkoani Ruvuma vilivyochukuliwa vinaonesha kuwa chanzo hicho ambacho kinamwaga maji yake mto Ruvuma kina kiwango kikubwa cha zebaki ambacho ni 0.02(Hg) ambapo kiwango cha kawaida kinachokubalika ni 0.005(Hg).
Vipimo vya maabara za uchunguzi wa maji vilivyochukuliwa kati ya mwaka 2008 hadi 2010 ,vilibaini kuwa maji hayo licha ya kuwa na kiwango kikubwa cha zebaki,pia yana kiwango kikubwa cha taka/tope(turbidity) ambacho kinavuka kiwango kinachokubalika kitaifa na hata cha Shirika la Afya Duniani (WHO).
Kiwango cha taka ambacho kinakubalika kitaifa kinaelezwa kitaalam kuwa ni etu 30; kiwango cha kimataifa ni etu 5 – 25. Lakini maji ya chanzo hicho yana etu 1,141 jambo ambalo ni hatari.
“Hali ni mbaya zaidi kwenye maeneo ambayo mito inatoka machimboni na imeungana na mto Ruvuma hasa wilaya ya Namtumbo mkoani Ruvuma na Mkoa wa Mtwara,katika maeneo hayo mtu akila kuanzia samaki wanne wenye zebaki anaweza kuathirika kwa kuwa kemikali hiyo ni sumu’’,anasisitiza Challe.
Mwandishi wa Makala haya ni Albano Midelo
Afisa Habari Manispaa ya Songea
Baruapepe:albano.midelo@gmail.com,simu 0784765917
SONGEA MUNICIPAL COUNCIL
Anuani ya Posta: P O BOX 14, SONGEA
Simu ya Mezani: 025 2602970
Simu ya Kiganjani:
Barua Pepe: info@songeamc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Manispaa ya Songea. Haki zote zimehifadhiwa