TAIFA letu bado limo katika tatizo la ujinga wa kutojua kusoma na kuandika.Serikali za awamu ya kwanza,ya pili, ya tatu, ya nne na sasa ya tano zimefanya mipango thabiti ya utoaji elimu ambapo hivi sasa kuna mpango wa elimu bure kuanzia shule ya msingi hadi kidato cha nne,hata hivyo mpango wa kufufua upya kisomo cha kujiendeleza bado changamoto ni kubwa.
Kwa mujibu wa matokeo ya sensa ya watu na makazi iliyofanyika mwaka 2002,kulikuwa na watu wazima milioni 5.5 katika nchi nzima sawa na asilimia 32 ya watu ambao hawajui kusoma, kuandika na kuhesabu.
Idadi ya watu wasiojua kusoma na kuandika imeendelea kuongezeka na kufikia zaidi ya watu milioni 10 kwa mujibu wa sensa ya watu na makazi ya mwaka 2012.Wakati kiwango cha watu wazima wasiojua kusoma kuandika na kuhesabu kikiongezeka mwaka hadi mwaka hapa nchini,taarifa ya utafiti ya kimataifa inasema bado kuna watu wazima milioni 750 duniani wasiojua kusoma,kuandika na kuhesabu.
Shirika la Umoja wa Mataifa linalohusika na Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO) linabainisha idadikubwa ya watu hao ambao hawajui kusoma, kuandika na kuhesabu wanaishi katika mabara ya Afrika na Asia.Ripoti ya UNESCO inaonesha kuwa robo tatu ya watu wasiojua kusoma na kuandika ni wanawake,
Hotuba ya Waziri wa Elimu wa Zamani Dk. Shukuru Kawambwa ya mwaka 2013 katika warsha ya Mpango wa Matokeo Makubwa Sasa kwa watendaji wa elimu ngazi ya Kanda,Mkoa na Wilaya alishangazwa na kuwepo wanafunzi wanaofika mpaka darasa la saba pasipokujua kusoma na kuandika.
“Halafu Afisa Elimu unawateua wanafunzi wa aina hiyo kwenda Sekondari.Tatizo liko wapi? Uteuzi wenu unazingatia vigezo vipi? Je hakuna namna ya kuthibitisha wale waliochaguliwa iwapo wanajua kusoma na kuandika?’’,alihoji Dk.Kawambwa.
Hata hivyo sera mpya ya elimu na mafunzo ya mwaka 2014 dhima yake ni kuinua ubora wa elimu na mafunzo na kuweka mifumo na taratibu zitakazowezesha kupata idadi kubwa ya Watanzania walioelimika na wanaopenda kujielimisha zaidi ili waweze kuchangia katika kufikia malengo ya maendeleo ya Taifa letu.
Wataalam duniani kote uhusisha elimu hafifu na umasikini na upeo mkubwa wa elimu na utajiri.Tafiti zimebaini kuwa sehemu ambazo idadi kubwa ya watu wana elimu ndogo kiwango cha umasikini ni kikubwa na maeneo ambayo wananchi wengi wana elimu ya kutosha huwa na maendeleo makubwa kiuchumi, kijamii,kiutamaduni na kisiasa.
Ikumbukwe kuwa Tanzania iling’ara katika Bara lote la Afrika, hasa Kusini mwa Jangwa la Sahara, miaka ya 1970 na 1980, kutokana na kupunguza kwa kasi idadi ya wananchi wake wasiojua kusoma na kuandika.Hadi Baba wa Taifa Mwl.Julius Nyerere anaondoka madarakani,takwimu zinaonesha kuwa idadi ya watanzania waliokuwa hawajui kusoma na kuandika ilikuwa takribani asilimia tisa tu.
Wataalam wanabainisha kuwa kuongezeka kwa idadi kubwa ya watu wanaojua kusoma na kuandika kungesababisha watanzania kufikiria mambo makubwa ya ugunduzi, uvumbuzi viwanda na teknolojia ya hali ya juu.Mwaka 1964 msisitizo ulikuwa elimu kwa wote na Mwaka 1970 Msisitizo wa elimu ya watu wazima ulitangazwa na hayati Mwalimu Nyerere kuwa suala la kuelimisha watu wazima ni jukumu la kila Mtanzania aliyekuwa anajua kusoma na kuandika.
Serikali ya awamu ya tano inatekeleza mpango wa elimu bure kuanzia Januari 2016 ambapo idadi ya wanafunzi walioandikishwa darasa la kwanza na kidato cha kwanza imeongezeka kwa kasi ya kutisha ambapo baadhi ya shule wameandikishwa hadi wanafunzi 700 hadi 900 kwa shule moja kuanza darasa la kwanza.
Ongezeko hili linadhihirisha kuwa kulikuwa na idadi kubwa ya wanafunzi waliostahili kuandikishwa darasa la kwanza lakini wazazi na walezi wao walishindwa kumudu gharama za kuandikishwa shule hivyo wengi walikuwa hawasomi na kusababisha idadi ya watu wasiojua kusoma na kuandika kuongezeka kila mwaka.
Elimu bora ndiyo inayomwezesha mtu kuyatumia mazingira yanayomzunguka ili kuboresha maisha yake.Ndani ya utandawazi, elimu isiyotosheleza, tafsiri yake ni umaskini zaidi;wakati elimu zaidi tafsiri yake ni maisha bora zaidi.
Mwandishi wa makala haya ni Albano Midelo anapatikana kwa kwa baruapepe:albano.midelo@gmail.com,simu,0784765917
SONGEA MUNICIPAL COUNCIL
Anuani ya Posta: P O BOX 14, SONGEA
Simu ya Mezani: 025 2602970
Simu ya Kiganjani:
Barua Pepe: info@songeamc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Manispaa ya Songea. Haki zote zimehifadhiwa