Ruhira hifadhi pekee nchini ya asili iliyopo mjini
MOJA ya vivutio vikubwa vya utalii katika mkoa wa Ruvuma ni hifadhi ndogo ya asili ya wanyama inayoitwa Ruhila Natural Game Reserve yenye ukubwa wa hekta 600 ambayo ilianzishwa mwaka 1973,ipo umbali wa kilometa saba kutoka Mmjini Songea. Ndani ya Hifadhi hiyo kuna aina mbalimbali za wanyama wakiwemo pundamilia, fisimaji, nyani,pongo tumbili, kakakuona,swalapala na kobe,pia bustani hiyo ni makazi ya reptilia na ndege wa aina mbalimbali. Msimamizi Mkuu wa Hifadhi hiyo ambaye pia ni Mkuu wa Kikosi dhidi ya Ujangili Kanda ya Kusini Obeld Mmari anasema ndani ya Hifadhi ya Luhira kuna aina mbalimbali za mimea ya asili ikiwemo miombo, minyonyo, mining, mikusu, migunga,miwanga,mizambarau,mirama,mitunduru,misasa,mi viru na mikuyu. “Ndani ya Luhira,mtalii anaweza kufanya utalii wa kutembea kwa miguu,kupiga picha,kuangalia wanyama na ndege,utalii wa kuweka kambi(camping) na kufanya mapumziko ya mchana(picnic) hufanyika ndani ya eneo maalum’’,anasema. Kumbukumbu zinaonesha kuwa wakati hifadhi hiyo
inaanzishwa ilikuwa mbali na makazi ya binadamu ambapohivi sasa ipo umbali wa kilometa sifuri na makazi ya watu.
Msimamizi Mkuu wa Hifadhi hiyo ambaye pia ni Mkuu wa Kanda ya Kusini wa Kikosi dhidi ya Ujangili Obeld Mmari anasema kutokana na uharibifu,huo wa mazingira uliosababishwa na shughuli za kibinadamu wakazi wanaoishi jirani na hifadhi hiyo wamekuwa wakitegemea uoto wa asili uliohifadhiwa katika hifadhi hivyo kuhatarisha uwepo wake. Kulingana na Mmari,hifadhi hiyo wakati inaanzishwa kulikuwa na wanyama na ndege mbalimbali ukiachilia mbali mimea na mito kama vile kapala, nakuchundu, nakala na mto Ruhila ambao ndiyo chanzo cha hifadhi hiyo kuitwa jina la Ruhila.
Hifadhi hiyo imezungukwa na mitaa mitatu iliyopo katika Manispaa ya Songea ambayo ni Mkuzo,Chandarua na Mshangano. Historia ya hifadhi hiyo inaonesha kuwa baada ya hifadhi hiyo kuanzishwa,mwaka 1974 walichukuliwa wanyamapori toka Arusha ambao ni pofu waliletwa tisa ambao hivi sasa hawapo na nyumbu tisa ambao pia hivi sasa hawapo. Wanyama wengine ni kuro mmoja ambaye hivi sasa hayupo na pundamilia waliletwa 10 kutoka Arusha ambapo hivi sasa katika hifadhi hiyo wamebakia pundamilia watano. Shughuli ya kuwaleta wanyama hao kutoka Arusha ilifanyika mwaka 1975 chini ya Mhifadhi Hashimu Sariko ambaye ni Meneja Mstaafu wa pori la akiba la wanyamapori Liparamba wilayani Nyasa Mkoa wa Ruvuma. Kabla ya wanyama hao kuletwa kutoka Holding Ground ya Orodonyosambu mkoani Arusha kulijengwa fensi katika hifadhi ya Ruhila ambayo ilisimamiwa na Ngwatura Ndunguru Afisa Maliasili Mstaafu ambaye pia alikuwa Mbunge wa jimbo la Mbinga Mashariki katika kipindi cha mwaka 2000 hadi 2005.
Kumbukumbu za Hifadhi ya Ruhila za mwaka 1981 zinaonesha kuwa wanyama hao waliongeeka ambapo pofu waliongezeka toka tisa hadi 15. Kulingana na kumbukumbu hizo,pundamilia waliongezeka toka 10 hadi 26,nyumbu waliongezeka toka tisa hadi 13,kuro alibakia mmoja ngorombwe waliongezeka toka watatu hadi watano na chatu wameendelea kuongezeka kwa wingi kila
mwaka.
Hata hivyo Muongozaji watalii katika Hifadhi ya Ruhila Mhifadhi Salvatory Salvatory ametahadharisha kuwa ndege aina ya kanga wameanza kupungua katika hifadhi hiyo hali ambayo anasema inahatarisha maisha ya chatu ambao hutegemea sana mayai ya kanga na vifaranga. Salvatory anasema idadi ya watalii wanaotembelea hifadhi hiyo kwa ajili ya utalii wa mafunzo(study tours) imekuwa inaongezeka kila mwaka huku idadi kubwa wakiwa ni watalii wa ndani.Anasema lengo ni kuhamasisha wanafunzi na walimu kutembelea hifadhi hiyo ambayo ipo mjini ili kujenga moyo wa kufanya utalii. “Watalii kutoka nje ya nchi pia wanatembelea hifadhi yetu,mwaka 2016 na mwaka huu tumepokea watalii toka Ujerumani,Afrika ya Kusini,India,Ufaransa,Italia, Uholanzi na wageni toka mikoa mbalimbali nchini,wanafanya utalii wa kuchunguza aina ya mimea na ndege’’,anasema Salvatory. Hata hivyo Mkuu wa Kikosi dhidi ya Ujangili Kanda ya Kusini anasema wanatarajia kupima eneo lote la hifadhi ili kupata hatimiliki ambayo itawawezesha kuongeza uwekezaji katika hifadhi hiyo sanjari na kuongeza idadi ya wanyama ili kuvutia watalii wengi wa ndani na nje. “Tunajiandaa kuweka mazingira ambayo yatawezesha wanyama kama tembo,simba na wanyama wengine adimu kuishi katika hifadhi yetu bila kuleta athari kwa wanyama wenyewe na binadamu hivyo ni vema kufanya utafiti kwanza na kupima kisayansi uwezo wa eneo la hifadhi kama wanyama hao wanaweza kuishi’’,anasisitiza Mhifadhi Mmari. Anasema hivi karibuni Hifadhi hiyo imetumia zaidi ya sh. Milioni 15 kuleta wanyama aina ya swalapala watano na pongo wawili toka Hifadhi ya Arusha hivyo anasisitiza kuwa kuongeza wanyama inahitajika sanyansi,fedha na utalaamu. Mmari anazitaja changamoto zinazoikabili hifadhi hiyo ndogo ya wanyama kuwa ni ubovu wa barabara ya kwenda hifadhini yenye urefu wa kilometa 3.5 toka mjini Songea. “Nashauri barabara hiyo ifanyiwe matengenezo kwa kuwa ina mashimo mengi,ikiwezekana kupandishwa tuta,kuweka changarawe au kuweka lami hali ambayo itavutia watalii wengi kutumia muda mfupi kufika hapa’’anasema Mmari.
Changamoto nyingine anaitaja kuwa ni nyumba za watumishi wa hifadhi hiyo zinahitaji kukarabatiwa kwa kuwa kumbukumbu zinaonesha kuwa tangu nyumba hizo zijengwe kati ya mwaka 1973 hadi 1974 hazijawahi kufanyiwa ukarabati mkubwa. Katika kuhakikisha watendaji wa hifadhi na wananchi wanajenga ushirikiano mzuri,Mmari anasema kuwa amefanya vikao mbalimbali na wananchi wanaozunguka eneo la hifadhi wakiwemo wazee na viongozi wa mitaa kwa nia ya kutengeneza mazingira mazuri ya ujirani mwema,kusikiliza matatizo yao na kutoa elimu ya uhifadhi na faida za utalii.
Anasema juhudi za makusudi zimechukuliwa kukarabati fensi inayozunguka hifadhi hiyo hali ambayo inawafanya wanyama kutoweza kutoka nje ya hifadhi,kula mazao ya wananchi na kuwa katika hatari ya kuuawa na majangili. “Ofisi yangu imetenga maeneo yanayofaa kuweka camp site,kuchonga barabara kwa ajili ya kupita wageni pia kukinga moto usioratibiwa,ndani ya hifadhi tuna vyoo vya kisasa kwaajili ya wageni na askari wanapokuwa zamu, tunaendelea kuanisha maeneo mengine ili kuboresha huduma’’,anasisitiza Mmari.
Anasisitiza zaidi kuwa ili kukimbizana na muda katika suala la utalii ameandikiwa Mkurugenzi Msaidizi wa Idara ya Wanyamapori Mafunzo kumuomba wanafunzi wanaosoma katika Chuo cha Mweka wafike kusini ili kufanya elimu ya vitendo katika hifadhi ya Ruhila na maeneo mengine ambazo anasema zitasaidia kupanga na kuboresha mipango ya utalii kusini.
Anayataja majukumu ambayo yapo katika mtizamo wa hifadhi shirikishi na endelevu kuwa ni kuhifadhi wanyamapori, kulinda maisha ya wananchi,kulinda mazao na mali za wananchi wanaozunguka maeneo ya hifadhi.
Hifadhi ya asili ya Ruhila,inafikika kwa urahisi kwa ndege au kutumia barabara ya Njombe hadi Songea ambayo ni ya lami,ukifika Songea mjini eneo la Msamala kuna barabara ya vumbi kiasi cha kilometa 3.5 unakuwa umefika bustani ya Luhira. Malazi ya wageni yanapatikana Manispaa ya Songea ambapo wageni pia wanaweza kuweka mahema ya muda katika maeneo yaliyotengwa ndani ya hifadhi hiyo.
Mwandishi wa makala haya ni Afisa Habari na Mawasiliano
wa Manispaa ya Songea anapatikana kwa simu
0784765917 barua pepe albano.midelo.com
SONGEA MUNICIPAL COUNCIL
Anuani ya Posta: P O BOX 14, SONGEA
Simu ya Mezani: 025 2602970
Simu ya Kiganjani:
Barua Pepe: info@songeamc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Manispaa ya Songea. Haki zote zimehifadhiwa