MOJA ya vivutio vikubwa vya utalii katika mkoa wa Ruvuma ni hifadhi ndogo ya asili ya wanyama inayoitwa Ruhila Natural Game Reserve yenye ukubwa wa hekta 600 ambayo ilianzishwa mwaka 1973,ipo umbali wa kilometa saba kutoka mjini Songea.
Ndani ya Hifadhi hiyo kuna aina mbalimbali za wanyama wakiwemo pundamilia, fisimaji, nyani,pongo tumbili, kakakuona,swalapala na kobe,pia bustani hiyo ni makazi ya reptilia na ndege wa aina mbalimbali.
Msimamizi Mkuu wa Hifadhi hiyo Msonda Simwanza anasema ndani ya Hifadhi ya Luhira kuna aina mbalimbali za mimea ya asili ikiwemo miombo, minyonyo, mininga, mikusu, migunga, miwanga, mizambarau, mirama, mitunduru,misasa,miviru na mikuyu.
“Ndani ya Luhira,mtalii anaweza kufanya utalii wa kutembea kwa miguu,kupiga picha,kuangalia wanyama na ndege,utalii wa kuweka kambi(camping) na kufanya mapumziko ya mchana(picnic) hufanyika ndani ya eneo maalum’’,anasema.
Historia ya hifadhi hiyo inaonesha kuwa baada ya hifadhi hiyo kuanzishwa,mwaka 1974 walichukuliwa wanyamapori toka Arusha ambao ni pofu waliletwa tisa ambao hivi sasa hawapo na nyumbu tisa ambao pia hivi sasa hawapo.
Kumbukumbu za Hifadhi ya Ruhila za mwaka 1981 zinaonesha kuwa wanyama hao waliongezeka ambapo pofu waliongezeka toka tisa hadi 15.
Kulingana na kumbukumbu hizo,pundamilia waliongezeka toka 10 hadi 26,nyumbu waliongezeka toka tisa hadi 13,kuro alibakia mmoja ngorombwe waliongezeka toka watatu hadi watano na chatu wameendelea kuongezeka kwa wingi kila mwaka.
Hata hivyo Muongozaji watalii katika Hifadhi ya Ruhila Mhifadhi Salvatory Salvatory anasema idadi ya watalii wanaotembelea hifadhi hiyo kwa ajili ya utalii wa mafunzo(study tours) imekuwa inaongezeka kila mwaka huku idadi kubwa wakiwa ni watalii wa ndani.Anasema lengo ni kuhamasisha wanafunzi na walimu kutembelea hifadhi hiyo ambayo ipo mjini ili kujenga moyo wa kufanya utalii.
“Watalii kutoka nje ya nchi pia wanatembelea hifadhi yetu,mwaka 2016 na mwaka huu tumepokea watalii toka Ujerumani,Afrika ya Kusini,India,Ufaransa,Italia, Uholanzi na wageni toka mikoa mbalimbali nchini,wanafanya utalii wa kuchunguza aina ya mimea na ndege’’,anasema Salvatory.
“Tunajiandaa kuweka mazingira ambayo yatawezesha wanyama kama tembo,simba na wanyama wengine adimu kuishi katika hifadhi yetu bila kuleta athari kwa wanyama wenyewe na binadamu hivyo ni vema kufanya utafiti kwanza na kupima kisayansi uwezo wa eneo la hifadhi kama wanyama hao wanaweza kuishi’’,anasisitiza Msonda.
Hifadhi ya asili ya Ruhila,inafikika kwa urahisi kwa ndege au kutumia barabara ya Njombe hadi Songea ambayo ni ya lami,ukifika Songea mjini eneo la Msamala kuna barabara ya vumbi kiasi cha kilometa 3.5 unakuwa umefika bustani ya Luhira.
Malazi ya wageni yanapatikana Manispaa ya Songea ambapo wageni pia wanaweza kuweka mahema ya muda katika maeneo yaliyotengwa ndani ya hifadhi hiyo.
Makala imeandikwa na
Albano Midelo
Afisa Habari Manispaa ya Songea
Mei 10,2018
SONGEA MUNICIPAL COUNCIL
Anuani ya Posta: P O BOX 14, SONGEA
Simu ya Mezani: 025 2602970
Simu ya Kiganjani:
Barua Pepe: info@songeamc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Manispaa ya Songea. Haki zote zimehifadhiwa