KESHO ni kilele cha maadhimisho ya Juma la mazingira ambayo kimkoa yanatarajia kufanyika katika Mtaa wa Mjimwema B Kata ya Mjimwema Manispaa ya Songea,ambapo mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Christina Mndeme.Kila mwaka wiki ya mazingira inafanyika kuanzia Mei 31 na kilele chake ni Juni 5.Kauli mbiu ya maadhimisho ya mwaka huu ni "Mkaa ni Gharama,Tumia Nishati Mbadala".Madhumuni ya ujumbe huu kitaifa unalenga kuelimisha matumizi ya nishati mbadala kwa wananchi ili kukabiliana na changamoto ya ukataji miti hovyo.
Wakati tunaadhimisha kilele cha siku ya mazingira,Uchafuzi na uharibifu wa mazingira ardhini,majini na nchi kavu umekithiri katika kiwango ambacho kinatishia kutoweka kwa sayari ya Dunia na viumbehai, endapo hatua za makusudi hazitachukuliwa kuinusuru hali hiyo.
Athari za mabadiliko ya hali ya hewa hapa nchini na duniani kote zinasababisha kila mwaka serikali kutenga bajeti ya zaidi y ash.trilioni 1.12 kukabiliana na athari za mazingira kutokana na mabadiliko ya hali ya hewa.
Kasi ya kutoweka kwa maji inaongezeka,tatizo la upatikanaji wa maji pia linaongezeka kutokana na kuongezeka kwa ukame unaosababishwa na shughuli za kibinadamu kwenye vyanzo vya maji.Tusipochukua hatua,Vita ya Dunia ya kugombania majii inakuja.
Wanasayansi wanasema shughuli mbalimbali za kibinadamu zimesababisha kuongezeka kwa joto la Dunia kwa nyuzi 0.85c na kusababisha madhara yote yanayotokea hivi sasa duniani yakiwemo ukame,magonjwa,mafuriko na mabadiliko ya tabianchi.
Hata hivyo wanasayansi wanatahadharisha kuwa iwapo joto duniani litaongezeka hadi kufikia nyuzi joto 1.5c ambalo ni ongezeko la nyuzi joto 0.65c viumbehai wote waliopo duniani hawataweza kumudu kuishi na hiyo itakuwa ndiyo mwisho wa vita kuu ya tatu ya Dunia ambayo itaangamiza Dunia nzima na viumbehai waliopo.
Kwa mujibu wa wanasayansi Mwaka 2012 ongezeko la joto duniani lilikuwa nyuzi 0.7c na kwamba kiwango cha joto kilifikia nyuzi 0.85c hadi kufikia mwaka 2015.
Moja ya sababu kuu zinazochangia kuendelea kuongezeka kwa hewa ya ukaa angani ni maendeleo ya viwanda ambavyo vinatoa moshi ambao unasambaa angani na kufanya uchafuzi mkubwa wa mazingira ya anga pamoja na moshi mwingi wa magari husababisha gesi ya ukaa kwenda moja kwa moja angani.
Utafiti mpya umeonesha kuwa watu milioni sita kote duniani wanakufa kila mwaka kutokana uchafuzi wa mazingira ya hewa ambapo asilimia 90 ya watu wote duniani wanavuta hewa chafu.
Ripoti ya Shirika la Afya Duniani (WHO) iliyotolewa Septemba 2016, inaeleza kuwa watu 9 kati ya 10 wanavuta hewa chafu duniani kote kila siku,hali inayoongeza hatari ya watu kuugua magonjwa mbalimbali yanayosababisha vifo vingi.
Mazingira salama ndiyo msingi wa uhai wetu,mazingira yakiwa na afya tutakuwa na afya,mazingira yakiugua tutaugua na mazingira yakifa viumbe wote tunafutika katika uso wa dunia.
Makala haya yameandaliwa na Albano Midelo
Afisa Habari Manispaa ya Songea
Juni 4,2018
SONGEA MUNICIPAL COUNCIL
Anuani ya Posta: P O BOX 14, SONGEA
Simu ya Mezani: 025 2602970
Simu ya Kiganjani:
Barua Pepe: info@songeamc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Manispaa ya Songea. Haki zote zimehifadhiwa