NA,
AMINA PILLY,
AFISA HABARI MANISPAA.
15.10.2021.
Halmashauri ya Manispaa ya Songea imeungana na Watanzania wengine katika kuadhimisha siku ya Mwanamke anayeishi Kijijini leo tarehe 15 Oktoba 2021.
Maadhimisho hayo yamefanyika katika kata ya Mwengemshindo Manispaa ya Songea na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali kutoka ndani ya Manispaa ya Songea wakiwemo Waheshimiwa Madiwani pamoja na Mwenyekiti wa UWT Wilaya ya Songea.
Mgeni rasmi katika maadhimisho hayo alikuwa ni Mstahiki Meya Manispaa ya Songea Michael Mbano ambaye alianza kwa kuwapongeza viongozi wa Manispaa ya Songea kwa kuratibu maadhimisho hayo ambayo yamefanyika kwa mara ya kwanza nchini Tanzania ambapo kitaifa yameadhimishwa Mkoani Kilimanjaro.
Mbano amewataka wanaume wote kuachana na mila na desturi potofu zinazowazuia wanawake hasa wanaoishi Kijijini kumiliki ardhi, kwa kuwaruhusu na kuwarithisha watoto wa kike haki sawa na vijana wa kiume katika suala zima la kumiliki ardhi kama hazina ya maisha yao ya baadae.
Amesisitiza kuwa maadhimisho haya yamelenga kufanya kampeni ya kumuwezesha mwanamke hasa anayeishi kijijini kuwa na haki ya kumiliki ardhi pamoja na kutoa nafasi ya pekee kwa mwananmke katika kukabiliana na ugonjwa wa UVIKO 19.”Alibainisha”
Amewataka wanawake kutumia nafasi yao kama fursa katika kukabiliana na ugonjwa wa UVIKO 19 kwa kuanza kutoa elimu kwenye familia zao namna ya kujikinga na kuandaa vifaa kinga kama vile maji tiririka, vitakasa mikono pamoja na barakoa n.k.
Ametoa wito kwa wanawake na wananchi wote wa Manispaa ya Songea kuendelea kujitokeza kwa wingi kupata chanjo ya Uviko 19 na amewatoa hofu wananchi kuhusiana upotoshaji wa jamii juu ya matumizi ya chanjo hiyo na kuwahakikishia usalama na umuhimu wa kutumia chanjo ili kujikinga na ugonjwa wa UVIKO 19.’Alisisitiza’
Naye Afisa maendeleo ya jamii Manispaa ya Songea Joyce Mwanja alibainisha kuwa, lengo la kuadhimisha siku hii ni kuwawezesha wanawake wanaoishi kijijini katika kukabiliana na changamoto ya UVIKO 19 pamoja na kuelimisha jamii juu ya haki ya mwanamke katika umiliki wa ardhi.
Aliongeza kuwa Wizara ya Maendeleo ya jamii, Afya, Jinsia, wazee na Watoto imeandaa siku hii maalumu ili kuelimisha jamii iweze kutambua nafasi ya mwanamke katika kukabiliana na UVIKO 19 kwa kutoa elimu na kuhamasisha juu ya njia mbalimbali za kujikinga na UVIKO 19 pamoja na uchomaji wa chanjo..
Maadhimisho hayo yaliadhimishwa na wananchi mbalimbali waliojitokeza kupata chanjo ya UVIKO 19 uwanjani hapo wakiongozwa na Diwani wa Kata ya Mwengemshindo Kapinga Osmund Sixmund.
Kauli mbiu katika maadhimisho ya Siku ya mwanamke anayeishi kijijini ni;
“TUJENGE USTAHIMILIVU KWA MWANAMKE ANAYEISHI KIJIJINI KATIKA KUKABILIANA NA UVIKO 19”
Mwisho.
SONGEA MUNICIPAL COUNCIL
Anuani ya Posta: P O BOX 14, SONGEA
Simu ya Mezani: 025 2602970
Simu ya Kiganjani:
Barua Pepe: info@songeamc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Manispaa ya Songea. Haki zote zimehifadhiwa