MKUU wa Mkoa wa Ruvuma Christina Mndeme amewaagiza madiwani wa Manispaa ya Songea kuhakikisha fedha zote zinazotolewa na serikali katika utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo zinatumika ipasavyo na kuchukua hatua haraka kwa watendaji pale ambapo itabainika kuwa fedha hizo zimetumika kinyume.
Mndeme ametoa maagizo hayo wakati anazungumza kwenye kikao maalum cha Baraza hilo cha kujibu hoja za mkaguzi wa Mahesabu kilichofanyika kwenye ukumbi wa Manispaa ya Songea.Amesema mwananchi yeyote ana haki ya kufaidika na fedha za serikali na kumchukulia hatua mtendaji yeyote ambaye atatumia fedha za serikali kinyume cha sheria za nchi.
Amesema madiwani wanastahili kuhoji endapo matumizi ya mfuko wa jimbo yametumika tofauti na ilivyopangwa na kwamba madiwani wanatekeleza ilani ya CCM hivyo wanasthili kujua iwapo fedha za serikali zimetumika vizuri au vibaya na kuchukua hatua haraka.
Hata hivyo Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma amewapongeza madiwani na watalaam kwa kuiwezesha manispaa hiyo kupata Hati ya kuridhisha kwa miaka miwili mfululizo na kusisitiza kuwa kupata Hati inayoridhisha kusiwafanye kubweteka na kujisahau kwa sababu ukaguzi wa hesabu za serikali unafanyika kila mwaka hivyo inatakiwa kumaliza mapungufu ya hoja za muda mrefu ambazo bado hazijafungwa ambapo Manispaa ina hoja ambazo bado hazijafungwa kwa kukosa majibu yanayojitosheleza.
Imetolewa na Albano Midelo
Afisa Habari Manispaa ya Songea
Julai 21,2018
SONGEA MUNICIPAL COUNCIL
Anuani ya Posta: P O BOX 14, SONGEA
Simu ya Mezani: 025 2602970
Simu ya Kiganjani:
Barua Pepe: info@songeamc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Manispaa ya Songea. Haki zote zimehifadhiwa