Na,
AMINA PILLY,
AFISA HABARI MANISPAA.
18.11.2021
Madiwani Halmashauri ya Manispaa ya Songea watakiwa kushiriki katika kusimamia utekelezaji wa miradi ya maendeleo katika maeneo yao.
Hayo yamebainishwa na Mkuu wa Wilaya ya Songea Pololet Kamando Mgema wakati akizungumza na Madiwani hao katika kikao cha baraza la Madiwani kilichofanyika leo tarehe 18 Novemba 2021 katika ukumbi wa Manispaa ya Songea kwa lengo la kujadili na kupanga mipango mbalimbali ya maendeleo ndani ya Halmashauri ya Manispaa ya Songea.
Mgema alisema kuwa katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo Madiwani wanayo nafasi kubwa kwa kusimamia na kuhakikisha kwamba miradi hiyo inatekelezwa katika maeneo yao kwa kiwango stahiki na muda maalumu uliopangwa na Serikali ambapo kwa Wilaya ya Songea miradi yote ya mpango wa maendeleo ya Taifa na mapambano dhidi ya UVIKO 19 inatakiwa kukamilika ifikapo tarehe 30 Novemba 2021.’Alisisitiza’
Naye Mstahiki Meya wa Manispaa ya Songea Michael Mbano alieleza kuwa miongoni mwa mikakati ya baraza hilo ni pamoja na kuboresha miundombinu ya barabara katika maeneo yaliyopo katikati ya mji ikiwemo na barabara ya mtaa wa Mahenge pamoja na kutoa mafunzo kwa Madiwani wa Manispaa ya Songea kuhusiana na mfuko wa afya ya jamii (CHF iliyoboreshwa) kwa lengo la kuongeza uelewa kwa Madiwani ili waweze kuwahamasisha wananchi kujiunga na mfuko huo.
Amewataka Madiwani wanapopanga bajeti ya maendeleo wazingatie vipaumbele vya wananchi ili kuweza kutatua changamoto zinazojitokeza katika utekelezaji wa mipango ya maendeleo katika Manispaa ya Songea.
Akijibu hoja iliyotolewa na Mheshimiwa Diwani kata ya Mletele Lungu Maurus Gerald kuhusiana na vituo vya mauzo ya mahindi, Mbano alisema kuwa hadi sasa katika Manispaa ya Songea mauzo ya mahindi yanafanyika katika kituo kimoja kilichopo Mwanamonga ambapo kila mwananchi anayetaka kuuza mahindi yake anatakiwa kupeleka katika kituo hicho.”Alibainisha”
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi Wilaya ya Songea Ally Abdallah Ally amewapongea waheshimiwa Madiwani na Viongozi wa Halmashauri ya Manispaa ya Songea kwa kufanya vizuri na kuweza kujenga vituo vya afya vingi ambavyo ni pamoja na kituo cha afya Subira, Lilambo na Mletele ambapo vitasaidia kutatua changamoto ya ukosefu wa huduma bora za afya katika maeneo hayo.
Amewataka Madiwani kuendelea kutimiza wajibu wao kwa kuzingatia utekelezaji wa Ilani ya chama cha mapinduzi pamoja na kushiriki katika kusimamia fedha zilizotolewa kwa ajili ya mpango wa maendeleo ya Taifa na mapambano dhidi ya UVIKO 19 zinatumika kwa matumizi stahiki na hilo litawezekana kwa kudumisha ushirikiano kati yao na wataalamu hasa kwenye suala zima la utekelezaji wa miradi hiyo kwa manufaa ya wananchi wao.
Mwisho.
SONGEA MUNICIPAL COUNCIL
Anuani ya Posta: P O BOX 14, SONGEA
Simu ya Mezani: 025 2602970
Simu ya Kiganjani:
Barua Pepe: info@songeamc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Manispaa ya Songea. Haki zote zimehifadhiwa