Mstahiki Meya Manispaa ya Mtwara /Mikindani Shadida Ndile amewaongoza Madiwani katika kutembelea Manispaa ya Songea kwa ajili ya kujifunza namna ya uendeshaji wa shughuli mbalimbali za maendeleo ikiwemo ukusanyaji wa mapato ya ndani ya Halmashauri.
Ziara hiyo imefanyika tarehe 23 Disemba 2022 katika Halmashauri Manispaa ya Songea ambapo walifanikiwa kutembelea Miradi mbalimbali ikiwemo Stendi mpya ya Mabasi Songea, Vikundi, Machinjio ya kisasa Songea pamoja na Kituo cha Afya Lilambo kilichojengwa kwa fedha za mapato ya ndani.
Ndile alisema Ziara yao imejaa mafanikio makubwa kutokana nakujifunza namna ya ukusanyaji wa mapato kwa kuweka wasimamizi kwa kila chanzo cha mapato ( Meneja) hali ambayo imepelekea kuongezeka kwa mapato ya Halmashauri, namna ya ukopeshaji wa mikopo kwa vikundi vya wanawake4%, Vijana 4%, na walemavu 2%, Usimamizi bora wa miradi ya maendeleo, na matumizi sahihi ya sheria ndogo za Halmashauri.
Amewataka Madiwani na Wataalam wote kuendelea kutoa ushirikiano katika kukusanya mapato pamoja na kuongeza ubunifu katika kuibua vyanzo mbalimbali vya Mapato ndani ya Halmashauri ili kufikia matarajio ya Serikali yaliyowekwa.
Aliongeza kuwa viongozi na wataalamu wanapaswa kuongeza ushupavu na uimara katika kutekeleza shughuli za Serikali ambazo zitasaidia kuonesha taswira nzuri na kuleta tija ya Maendeleo katika Halmashauri/Nchi kwa ujumla.
Naye Zuhura Mikidadi Diwani wa Viti maalmu Mtwara Mikindani alisema kupitia Ziara hiyo amejifunza namna ya uendeshaji wa machinjio ya kisasa, utoaji wa mikopo ya uwekezaji kwa vikundi (uwekezaji wa viwanda vidogo) na sio mikopo ya mtu mmoja mmoja ambayo haileti tija kwa jamii na kuahidi kutumia elimu hiyo kwa kuwafundisha wananchi wengine kupitia kata anayoiongoza.
Kwa upande wake Ahamadi Kalikumbe (Diwani ) alisema kuwa mafanikio yanayoonekana katika kutekeleza zoezi la ukusanyaji wa mapato ni ushirikiano baina ya waheshimiwa Madiwani na wataalamu na namna ya ukopeshaji wa vikundi, na ufuatiliaji wa madeni kwa wananavikundi waliokopeshwa.
Kwa upande Mstahiki Meya Michael Mbano alitoa shukrani na kuwakaribisha tena kuja kutembelea kwa mara nyingine kwa ajili ya kufanya tathimini kupitia shughuli walizojifunza ili kubaini mafanikio na changamoto wakati wa utekelezaji na usimamizi wa zoezi la ukusanyaji wa mapato kupitia vyanzo mbalimbali ikiwemo madini, vibali vya sherehe, lessen za vileo, na utoaji wa mikopo kwa vikundi.
IMEANDALIWA NA;
AMINA PILLY;
KITENGO CHA MAWASILIANO SERIKALINI.
SONGEA MUNICIPAL COUNCIL
Anuani ya Posta: P O BOX 14, SONGEA
Simu ya Mezani: 025 2602970
Simu ya Kiganjani:
Barua Pepe: info@songeamc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Manispaa ya Songea. Haki zote zimehifadhiwa