MADIWANI wawili wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo CHADEMA katika Halmashauri ya Manispaa ya Songea mkoani Ruvuma wamejiuzuru na wanatarajia kujiunga na chama tawala cha CCM.Mkurugenzi wa Manispaa ya Songea Tina Sekambo amethibitisha kupokea barua za kujiuzuru za madiwani hao wawili wa CHADEMA ambao amewataja kuwa ni Mheshimiwa Msosa Rashid Msosa aliyekuwa Diwani wa Kata ya Ruvuma na Mheshimiwa Mchungaji Martin Mrata aliyekuwa Diwani wa Kata ya Matarawe.
Alipoulizwa sababu za kujiuzuru aliyekuwa Diwani wa Kata ya Ruvuma,mheshimiwa Msosa amesema amesukumwa na kasi ya maendeleo ambayo inafanywa na Rais wa Awamu ya tano Dkt.John Magufuli ambapo amesema serikali imechangia miradi katika kata yake ukiwemo mradi wa ujenzi wa Kituo cha Afya Kata ya Ruvuma ambacho serikali imetoa shilingi milioni 400 katika hatua za awali za mradi huo.
"Kwa hiari yangu bila kusukumwa na mtu yeyote,nimeamua kujiuzuru CHADEMA na sasa kuhamia CCM,hivyo kwa sasa Kata ya Ruvuma haina Diwani,Rais Magufuli anafanyakazi kazi nzuri kwa ajili ya watanzania wote hivyo nimemua kumuunga mkono kwa kuhamia CCM'',amesisitiza Msosa.
Hata hivyo madiwani wote wawii leo wamehudhuria mkutano wa Baraza maalum la madiwani uliofanyika kwenye ukumbi wa Manispaa ya Songea na kuongozwa na Mwenyekiti ambaye pia ni Mstahiki Meya wa Manispaa ya Songea Alhaj Abdul Hassan Mshaweji.
Imetolewa na Albano Midelo
Afisa Habari Manispaa ya Songea
Septemba 21,2018
SONGEA MUNICIPAL COUNCIL
Anuani ya Posta: P O BOX 14, SONGEA
Simu ya Mezani: 025 2602970
Simu ya Kiganjani:
Barua Pepe: info@songeamc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Manispaa ya Songea. Haki zote zimehifadhiwa