MAMLAKA ya Udhibiti wa Chakula na Dawa(TFDA) chini ya Idara ya Afya na Ustawi wa Jamii katika Manispaa ya Songea mkoani Ruvuma imeyafungia maduka ya dawa muhimu 48 kutokana na kushindwa kukidhi vigezo vya uendeshaji wa maduka hayo.
Mganga Mkuu wa Manispaa ya Songea Dk.Mameritha Basike amesema Idara ya Afya imefanyakazi ya utambuzi wa maduka ya dawa muhimu ili kubaini iwapo maduka hayo yanakidhi vigezo kulingana na mwongozo wa uendeshaji wa maduka ya dawa muhimu nchini.
Amesema kati ya maduka hayo yaliyofungiwa, maduka sita yamegundulika yanaendeshwa bila kibali na maduka 12 hayafanyikazi kwa zaidi ya mwaka mmoja licha ya kuwa na vibali vya kuendesha ya dawa muhimu.
Kwa mujibu wa Dk.Basike,katika operesheni hiyo wameaini maduka nane hayajahuisha vibali vya dawa muhimu kwa zaidi ya mwaka mmoja na maduka 22 yamefunguliwa katikati ya mji wa Songea kinyume cha muongozo ya maduka ya dawa muhimu.
Hata hivyo amesema imebainika maduka 23 bado hayajapata kibali cha Mfamasia isipokuwa yana barua iliyotolewa na Ofisi ya Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Songea ya kuruhusiwa kuendesha biashara ya duka la dawa muhimu.
“Kati ya maduka ya dawa muhimu 222 yaliopo katika Halmashauri ya Manispaa ya Songea,ni maduka 146 ndiyo yana vibali vya kuendeshea biashara ya maduka ya dawa muhimu’’,anasema Dk.Basike.
Ameongeza kuwa katika operesheni ya utambuzi huo, maduka manne yamefungwa kwa sababu wamiliki wake wamefariki,wamiliki 11 wamiliki wake wamepewa muda wa miezi sita wa maduka yao kupandishwa hadhi kuwa maduka ya dawa moto(famasi) kwa kuwa maduka yao yalifunguliwa mwaka 2003 kabla ya sheria ya TFDA ya mwaka 2003.
Manispaa ya Songea imefanya utambuzi huo ili kutekeleza agizo la Katibu Mkuu Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa(TAMISEMI) ya kuyatambua maduka ya dawa muhimu na rejareja yaliyosajiriwa chini ya Baraza la Famasia yanayoendeshwa kisheria.
Katika agizo hilo Katibu Mkuu ameagiza kuyaondoa kwa kuyafunga mara moja maduka yote ya dawa muhimu katika maeneo ya miji mikubwa yalioanzishwa kinyume cha sheria.
Imetolewa na Albano Midelo
Afisa Habari Manispaa ya Songea
SONGEA MUNICIPAL COUNCIL
Anuani ya Posta: P O BOX 14, SONGEA
Simu ya Mezani: 025 2602970
Simu ya Kiganjani:
Barua Pepe: info@songeamc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Manispaa ya Songea. Haki zote zimehifadhiwa