Na,
AMINA PILLY,
AFISA HABARI MANISPAA.
02 MACHI 2022.
Halmashauri ya Manispaa ya Songea ina jumla ya idadi ya walengwa wanaopokea ruzuku ya kaya maskini 5,694, ikiwa miongoni mwa kaya hizo ni 2,625 ambazo zinalipwa fedha taslimu, kaya 2076 zinalipwa kwa mtandao na kaya 993 zinalipwa kwa OTC ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa mpango wa kunusuru kaya maskini (TASAF).
Hayo yamebainishwa na Kaimu Mkurugenzi wa Manispaa ya Songea Christopher Ngonyani ambaye pia ni Mratibu wa TASAF Manispaa ya Songea wakati akifungua mafunzo kwa wawezeshaji wa mamlaka za maeneo ya utekelezaji na usimamizi wa miradi ya kutoa ajira za muda chini ya mpango wa kunusuru kaya maskini – TASAF kwa awamu ya tatu kipindi cha pili yanayofanyika katika ukumbi wa Manispaa ya Songea leo tarehe 02 Machi 2022.
Alisema kuwa mafunzo hayo yamelenga katika kujenga uelewa kwa wawezeshaji juu ya namna ya kushirikiana na kuwasaidia wananchi kuibua miradi yenye tija ambayo itasaidia kuongeza kipato kwa walengwa hao.
Amewataka wawezeshaji hao kushiriki ipasavyo katika mafunzo hayo kwa muda maalumu uliopangwa, ambayo yanatarajiwa kufanyika kwa muda wa siku 6.
Akitolea ufafanuzi kuhusiana na mafunzo hayo, Afisa miradi ajira za muda TASAF, Abel Bimbiga alisema kuwa lengo la miradi hiyo ni kutoa fursa za ajira kwa kaya maskini, kutoa ujuzi kwa walengwa itakayowasaidia katika shughuli mbalimbali za maendeleo pamoja na kuwawezesha kupata miundo mbinu ambayo itatoa manufaa katika maeneo husika.
Aliongeza kuwa, mzunguko wa kwanza wa utekelezaji miradi hiyo ulifanyika katika Halmashauri 51 ikiwemo na Halamshauri ya Madaba, Songea vijijini pamoja na Tunduru ambapo katika mzunguko wa pili mradi utafikia Halmashauri 72 ikiwemo na Halmashauri ya Manispaa ya Songea.
“Aidha, Utaratibu wa kutoa mafunzo kwa wawezeshaji utasaidia katika usimamizi wa utekelezaji wa miradi hiyo ambapo zoezi la kuibua miradi litaanza ifikapo Aprili 2022 na utekelezaji wa miradi hiyo utaanzia mwezi Julai katika kipindi cha miezi 6” Bimbiga alibainisha.
Alisema kuwa miradi ya kutoa ajira za muda inalenga kutoa ajira kwa kaya maskini wakati wa kipindi cha hari ili wanakaya hao waweze kupokea ujira utakaowasaidia kuongeza kipato na hivyo kupunguza umaskini katika jamii.
Bimbiga alieleza kuwa katika kipindi cha kwanza cha mpango wa kunusuru kaya za walengwa jumla ya miradi 9,440 ya kutoa ajira za muda ilitekelezwa katika maeneo ya utekelezaji 44 kwa gharama ya shilingi bilioni 119 ambapo kati ya fedha hizo bilioni 83.3 ilitumika kwa ajili ya kulipa ujira kwa walengwa na shilingi bilioni 35.7 zilitumika kwa ajili ya ununuzi wa vifaa vya miradi na usimamizi.
Mwisho.
SONGEA MUNICIPAL COUNCIL
Anuani ya Posta: P O BOX 14, SONGEA
Simu ya Mezani: 025 2602970
Simu ya Kiganjani:
Barua Pepe: info@songeamc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Manispaa ya Songea. Haki zote zimehifadhiwa