MAKUMBUSHO ya Taifa ya Majimaji ni moja ya kivutio maarufu cha utalii katika Manispaa ya Songea mkoani Ruvuma ambacho kina utalii wa utamaduni na kishujaa.
Mhifadhi Kiongozi wa Makumbusho ya Taifa ya Majimaji Bartazar Nyamusya anasisitiza kuwa serikali imedhamiria kuyatangaza Makumbusho ya Taifa ya mashujaa wa vita Majimaji ili kufahamika ndani na nje ya nchi kutokana na makumbusho hayo kuhifadhi vifaa na silaha halisi ambazo walitumia mashujaa hao kupambana na wakoloni wa kijerumani.
“Hii ni Makumbusho pekee nchini ambayo imebahatika kuwa na vifaa vyote asilia na muhimu katika historia ya mtanzania hali ambayo inaitofautisha makumbusho hii na nyingine zilizopo hapa nchini ”,anasisitiza Mhifadhi huyo.
Anabainisha zaidi kuwa Mji wa Songea ni miongoni mwa miji michache nchini ambayo ilitoa upinzani mkali katika vita ya majimaji na kwamba katika makumbusho hayo kuna ushahidi ambao unaonesha moja kwa moja kuwa wazee wa Songea walishiriki kikamilifu katika vita hivyo.
Anabainisha zaidi kuwa katika eneo la mashujaa wa majimaji yamejengwa majengo mbalimbali ambayo yamehifadhiwa vifaa ambavyo vilitumiwa na mashujaa hao ili kuwaletea watanzania uhuru.
Ndani ya makumbusho ya Taifa ya Majimaji kuna mnara wa kumbukumbu ya wanajeshi ambao walitoka Songea kwenda kupigana vita vya Idd Amini kati ya mwaka 1978 hadi 1979 ambapo wakati wanarudi baada ya kushinda vita hivyo walipata ajali mbaya na kufariki dunia askari wote 56 katika milima ya Lukumbulu wilayani Songea.
Ili kuwakumbuka mashujaa hao serikali ilijenga mnara katika eneo Makumbusho ya Taifa ya Majimaji ambako walizikwa mashujaa wa vita vya majimaji kama sehemu ya kuwakumbuka.
Kulingana na sera ya utamaduni ya mwaka 1997 pamoja na sheria ambayo inayatambua maeneo haya serikali imeamua mji wa Songea uingizwe katika vivutio vya utalii wa kiutamaduni kwa ajili ya kuendeleza historia ya Mji wa Songea ili uwe wa kihistoria, kishujaa na kiutamaduni.
Mhifadhi Kiongozi wa Makumbusho ya Taifa ya Dar es salaam Philipo Maligisu anasema,utafiti uliofanywa na Makumbusho ya Taifa umebaini kuwa mji wa Songea una vigezo vyote vya kuingizwa katika rasilimali za kiutamaduni za taifa,ili kuhakikisha kuwa watalii wengi wa ndani na nje ya nchi wanafika katika makumbusho hayo kujifunza mambo mbalimbali ya historia ambayo ni urithi wa taifa letu.
Imeandaliwa na Albano Midelo
Afisa Habari Manispaa ya Songea
Mei 21,2018
SONGEA MUNICIPAL COUNCIL
Anuani ya Posta: P O BOX 14, SONGEA
Simu ya Mezani: 025 2602970
Simu ya Kiganjani:
Barua Pepe: info@songeamc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Manispaa ya Songea. Haki zote zimehifadhiwa