WATU 87 wamekufa kutokana na ugonjwa wa malaria katika Manispaa ya Songea mwaka 2016 sawa na asilimia 10.9 ya vifo vyote 798 vilivyotokana na magonjwa mengine.
Mganga Mkuu wa Manispaa ya Songea Dk.Mameritha Basike amesema kati ya vifo hivyo vifo vya watoto wenye umri chini ya miaka mitano vilikuwa ni 34 sawa na asilimia nane ya vifo vyote 401 vya watoto.
Takwimu za Manispaa hiyo katika kipindi hicho zinaonesha kuwa wagonjwa waliougua na kupata matibabu ya nje walikuwa ni 5,926 ambayo ni sawa na asilimia 2.4 ya wagonjwa wote 244,245 waliopata matibabu ya nje.
Dk.Basike amewataja wagonjwa waliougua malaria na kulazwa kwa mwaka 2016 kuwa walikuwa ni 6,042 sawa na asilimia 2.5 ya wagonjwa wote 244,425 waliolazwa.
“Ni dhahiri ugonjwa wa malaria huathiri zaidi watoto wenye umri chini ya miaka mitano na akinamama wajawazito kwa sababu katika kundi hili kinga za kupambana na malaria ni kidogo’’,anasema Dk.Basike.
Hata hivyo amesema katika Manispaa ya Songea bado ugonjwa wa malaria ni tatizo kubwa kwa sababu huchukua nafasi ya kwanza katika magonjwa 10 yanayoongoza kwa matibabu ya nje na ndani.
Kwa upande wake Afisa wa Afya katika Manispaa ya Songea Maxensius Mahundi amesema katika kukabiliana na malaria umilikaji wa vyandarua vyenye dawa ngazi ya kaya umeongezeka toka asilimia 65 mwaka 2015 hadi kufikia asilimia 75.1 mwaka 2016.
Amesema Halmashauri imetenga siku moja katika mwezi kwa ajili ya kufanya usafi wa mazingira ambapo wakazi wote toka kata 21 na mitaa 95 wanashiriki katika zoezi la usafi ikiwa ni njia mojawapo ya kupambana na malaria.
Hata hivyo Mahundi amesema kutokana na tatizo la malaria kuwa kubwa katika Manispaa ya Songea imewekwa mikakati mbalimbali ambayo ameitaja kuwa ni kuendeleza zoezi la ugawaji wa vyandarua bure katika jamii,kuendelea kununua dawa na kuendeleza tiba.
Mikakati mingine ni kuhamasisha upimaji,utoaji wa elimu kwa jamii,kufanya zoezi la utambuzi wa mazalia ya mbu kwenye kata na mitaa yote,kutoa mafunzo kwa watoa huduma na kuwachukulia hatua za kisheria wakazi wote wanaokiuka taratibu za usafi.
Naye Mstahiki Meya wa Manispaa hiyo Abdul Hassan Mshaweji amewashauri watalaam wa afya kutumia vyombo vya habari ili elimu dhidi ya ugonjwa wa malaria uweze kuwafikia wananchi ili wananchi waweze kuboresha mazingira ya makazi na kuwahi matibabu wanapoona dalili za malaria.
“Nawashauri wananchi kupima vimelea vya malaria kabla ya kupata matibabu,kuzingatia matumizi sahihi ya vyandarua vyenye dawa na Halmashauri kuhakikisha dawa za tiba zinapatikana wakati wote’’,anasema Mshaweji.
Siku ya malaria duniani huadhimishwa kila mwaka Aprili 25 ambapo kaulimbiu ya mwaka 2017 ni Shiriki Kutokomeza Malaria kabisa kwa Manufaa ya Jamii.
Taarifa imetolewa na
Albano Midelo
Afisa Habari na Mawasiliano Manispaa ya Songea
SONGEA MUNICIPAL COUNCIL
Anuani ya Posta: P O BOX 14, SONGEA
Simu ya Mezani: 025 2602970
Simu ya Kiganjani:
Barua Pepe: info@songeamc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Manispaa ya Songea. Haki zote zimehifadhiwa