Manispaa ya Songea ilivyodhamiria kuboresha na kuimarisha vyanzo vya mapato ya ndani
MAPATO ya ndani hayapokelewi kama yalivyo mapato mengine kama Fedha za matumizi mengineyo (OC) na Fedha za maendeleo au Fedha kutoka kwa wahisani. Mapato ya Ndani yanakusanywa kwa juhudi kubwa kwa kutumia rasilimali nyingi ili kuhakikisha yanakusanywa kwa wingi. Kiwango cha Mapato yanayokusanywa ni kipimo cha Juhudi na rasilimali zilizowekezwa katika ukusanyaji. Halmashauri ya Manispaa ya Songea katika Mkoa wa Ruvuma ipo katika mwendelezo wa uanzilishi, ustawishaji na Uimarishaji wa vyanzo vya Mapato ya Ndani. Katika Mchakato huo, Manispaa imechukua juhudi mbalimbali ikiwemo kuimarisha mfumo wa ukusanyaji na kuongeza nguvu kazi katika ukusanyaji na ufuatiliaji.
Mwekahazina Mkuu wa Manispaa ya Songea Joseph Mbiaji anasema Manispaa hiyo imekua ikipiga hatua katika ukusanyaji wa Mapato ya Ndani kila mwaka,ambapo Kwa miaka mitano iliyopita.
Halmashauri imefanikiwa kuongeza Mapato kwa asilimia 521.09 kutoka mwaka wa fedha 2011/2012 hadi 2015/2016. “Kwa mwaka huu wa fedha wa 2016/2017, Halmashauri inatarajia kukusanya sh. bilioni 3,368,465,000/= kutoka vyanzo vyake vya Ndani.Hadi kufikia 14.12.2016 Jumla ya sh. bilioni 1,120,633,737.98 sawa na asilimia 33.27 zimekusanywa’’, anasema Mbiaji. Anasema Halmashauri ya Manispaa ya Songea kama ilivyo kwa Taasisi nyingine zinazojihusisha na ukusanyaji wa Maduhuli (kodi mbalimbali) na utoaji wa huduma kwa Wananchi, imekuwa inakumbana na changamoto mbalimbali katika utekelezaji wa shughuli zake za kila siku. Anazitaja changamoto hizo kuwa ni baadhi ya wafanyabiashara kutolipa kodi na tozo za serikali,baadhi ya walipa kodi kutolipa kodi kwa wakati stahiki na baadhi ya wafanyabiashara kutoa taarifa zisizo sahihi ambazo husababisha tozo ndogo kuliko stahiki. Changamoto nyingine ni ukosefu wa elimu kwa baadhi ya walipa kodi na tozo za Halmashauri ikiwemo sheria ndogo za tozo mbalimbali,uwepo wa ukaidi wa makusudi kulipa kodi na tozo halali za Halmashauri kwa baadhi ya Wananchi na upotoshaji wa Tafsiri za viongozi kuhusu kufutwa kwa baadhi ya Mapato ya Halmashauri hasa ushuru mdogo mdogo.Salum Mwandu ni Afisa Mapato wa Manispaa ya Songea anasisitiza kuwa Halmashauri ya Manispaa ya Songea imepiga hatua katika ukusanyaji wa mapato kupitia njia mbalimbali za ndani na nje ya Manispaa zilizosababisha kufikia malengo ya ukusanyaji mapato. Anazitaja njia hizo kuwa ni matumizi ya mfumo wa kielekroniki katika ukusanyaji wa mapato ya Ndani (The Local Government Revenue Collection Information System (LGRCIS). Mwandu anasema Mfumo wa LGRCIS ndiyo mfumo pekee uliopitishwa nakupendekezwa na Wizara ya Fedha na Uchumi kutumika katika ukusanyaji wa Mapato kwa Halmashauri zote nchini. “Mfumo huo umekubalika kutokana na tija zilizopatikana katika Mamlaka za Miji, Manispaa na Majiji pamoja na ufanisi wake katika uwezo wa kuunganishwa na watoa huduma wengine kama vile Mabenki na Makampuni ya Simu katika kurahisisha Malipo ya tozo za Serikali’’,anasisitiza Mwandu.Ofisa Mapato huyo anaitaja njia nyingine ya ukusanyaji mapato kuwa ni matumizi ya Mashine katika ukusanyaji wa mapato yaani Point Of sale (POS) ambapo mashine za kieletroniki zinatumika katika ukusanyaji waMapato na kutoa stakabadhi kwa mlipaji wa huduma au tozo badala vitabu vya kawaida vilivyokuwa vinatumika awali.
Anabainisha kuwa Mashine hizo zimeunganishwa na mfumo wa mapato wa LGRCIS ambapo mkusanyaji wa Mapato hufahamika makusanyo yake hata kama hajafika kuwasilisha. Anasema Mashine hizo zimewezesha kuondoa changamoto za mawasilisho ya fedha na kuongeza uadilifu kwa wakusanyaji.
Kwa mujibu wa Afisa Mapato huyo Halmashauri ya Manispaa ya Songea ina jumla ya POS 30 ambazo zinatumika katika vyanzo mbalimbali ikiwemo Masoko, Maegesho, Stendi, Machinjio na Ushuru wa Mazao ya Misitu na Nafaka. Kuhusu ukusanyajiwa wa takwimu za Mapato,Mwandu anasema Halmashauri ya Manispaa ya Songea imefanikiwa kukusanya takwimu za walipa kodi na kutumia katika ukadiriaji wa Mapato katika vyanzo vyake vya Ndani.Anataja matumizi ya takwimu kwamba yanasaidia katika ukadiriaji wa Mapato na tathmini ya ukusanyaji kwenye kila chanzo ikiwemo Masoko,Magari na Malori yanayoingia Mjini na Magari yanayotumia stendi.
Mwekahazina Mkuu wa Manispaa ya Songea Joseph Mbiaji anaitaja mikakati ya kuongeza mapato ni kuhakikisha Idara na Halmashauri zinafanikisha malengo ya ukusanyaji Mapato ya Ndani, ikiwemo kuimarisha mfumo wa ukusanyaji wa mapato. “TAMISEMI imesimika mfumo wa kukusanyia Mapato ambapo Halmashauri inaendeleakuutumia na kuutunza kwa ajili ya kufikia malengo ya serikali katika kukuza ukusanyaji wa mapato ya ndani kamainavyoelekeza na viongozi wa Nchi’’,anasisitiza Mbiaji. Hata hivyo anasema Manispaa inatarajia kuongeza vitendea kazi katikaukusanyaji Mapato kwa kuwa shughuli za ukusanyaji mapato zinaenda sanjari na uwepo wa vifaa vya kukusanyia Mapato kama vile Gari, Pikipiki na Mashine za kukusanyia (POS),ambapo hivi sasa kitengo cha Mapato kina gari moja na Pikipiki moja tu, ambapo ongozeko la vifaa hivyo vitaongeza ufanisi.
Mkurugenzi wa Manispaa ya Songea Tina Sekambo anaitaja mikakati mingine ya kuimarisha ukusanyaji wa mapato ya ndani kuwa ni kuajiri wakusanyaji Mapato. Sekambo anabainisha kuwa tayari Halmashauri ya manispaa hiyo imeajiri wakusanya Mapato 14 ambao wamepangiwa maeneo mbalimbali kufanya kazi hiyo, na kwamba ni matarajio ya Manispaa hiyo kuongezeka Mapato kupitia mpango huo. Anasema ili kukisia na kukusanya Mapato kwa uhakika Takwimu za vyanzo na walipa kodi ni muhimu ili Halmashauri ifikie malengo kwa urahisi,ambapo Idara ya fedha itashirikiana na Idara nyingine kuhoisha takwimu mbalimbali zinazoweza kutoa taswira ya mwelekeo wa Mapato na walipa kodi. Sekambo anasema Manispaa inaboresha mfumo wa taarifa kwa walipa kodi ambapo Kitengo cha Mapato kimekuwa kinatunza taarifa za walipa kodi kwa kila chanzo,na kwamba mfumo wa utunzaji wa taarifa hizoutaboreshwa zaidi ili kuhakikisha zinasaidia katika kuongeza ufanisi wa ukusanyaji, utoaji wa taarifa sahihi na kuimarisha mawasiliano kwa wafanya biashara. Anasema Halmashauri itaendelea kutoa Elimu na taarifa sahihi kwa wadau pamoja na walipa kodi ili kupunguza mvutano na ukaidi kutoka kwa wadau wake,kutokana na wimbi la kupinga kulipa kodi au kutoa ushirikiano kwa wakusanyaji wa kodi hivyo kuwa kikwazo kwa ongezeko la Mapato.
Halmashauri ya Manispaa ya Songea imekusudia kujenga mahusiano ya kiutendaji na kubadilishana taarifa muhimu za wateja na watumiaji huduma zitolewazo na Mashirika , Taasisi, Asasi, Jumuiaya au Idara ili kuimarisha mahusiano na wadau pamoja na taasisi nyingine. Tayari Manispaa imefanya kongamano la siku mbili la kuibua vyanzo vipya vya mapato na kuboresha vyanzo vilivyopo.Kongamano hili imewashirikisha wadau mbalimbali wakiwemo wafanyabiashara,wakuu wa idara na vitengo vya Manispaa,madiwani,maafisa watendaji wa kata na mitaa,asasi za kifedha,viongozi wa Chama tawala na wadau wengine. Katika Juhudi za kuongeza Mapato ya Ndani,Manispaa ya Songea ina utaratibu wa kuongeza vyanzo vya Mapato kwa lengo la kupanua wigo wa ukusanyaji ili kungeza pato la Ndani. Mwekahazina Mkuu anavitaja vyanzo vipya vya mapato ambavyo vimebuniwa kuwa ni tozo za ulazaji wa Malori Makubwa Mjini Songea kwa kuwa imeonekana fursa ya Mapato kwa Malori ambayo yanalala maeneo ya Mjini kupitia maeneo ya kulaza Magari yakingojea kuanza safari, kupakia au kushusha Mizigo. Anasema kupitia chanzo hicho inatarajia kuwepo kwa zaidi ya Malori hamsini hulala ndani ya Manispaa kwa siku, hivyo kama Halmashauri itatoza Tshs 2000 kwa lori itaweza kukusanya Jumla ya sh.milioni 365,000,000 kwa mwaka. Anasema manispaa inatarajia kuanzisha Minada na Magulio katika
maeneo Mengine ili kupanua Mji na kuongeza Mapato, ambapo Halmashauri na wafanyabiashara wanatarajia kuanziasha Magulio kwa awamu kwa lengo la kukuza Mji na kuongeza chachu ya Maendeleo. “Kupitia uanzishwaji wa Magulio na Minada ni hakika makusanyo ya tozo, kodi na Ushuru wa huduma mbalimbali utaongezeka maradufu.Ongezeko la makusanyo katika maeneo hayo itategemea na mwitikio wa wafanyabiashara na wateja wa bidhaa zinazotolewa maeneo husika’’,anasisitiza Mbiaji.
Albano Midelo ni Mchangiaji wa Tovuti hii anapatikana kwa
baruapepe:albano.midelo@gmail.com,simu 0784765917
SONGEA MUNICIPAL COUNCIL
Anuani ya Posta: P O BOX 14, SONGEA
Simu ya Mezani: 025 2602970
Simu ya Kiganjani:
Barua Pepe: info@songeamc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Manispaa ya Songea. Haki zote zimehifadhiwa