HALI ya upatikanaji wa chakula katika Halmashauri ya Manispaa ya Songea mkoani Ruvuma ni nzuri ambapo jumla ya hekta 24,340.8 zililimwa msimu wa 2016/2017 na kuzalisha tani 98,671.76. wakati mahitaji ya chakula ni tani 58,280 hivyo kufanya kuwa na ziada ya tani 40,391.76 sawa na asilimia 69.3
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya songea Tina Sekambo amesema Manispaa hiyo inazalisha zao la Kahawa kama zao kuu la biashara ambapo manispaa imeweka mpango wa kuotesha miche ya kahawa 143,384 katika vitalu sita kwa msimu wa 2018/2019.
" Miche 121,784 inatarajiwa kupandwa katika ukubwa Hekta 72.94 na wakulima 290 watanufaika.Hali hii itasaidia kuboresha na kuinua kipato cha wananchi katika kaya zao'',amesisitiza Sekambo.
Ameyataja mazao mengine ya biashara yaliyozalishwa katika msimu wa 2016/2017 ni; Alizeti tani 182, Ufuta tani 32.5, karanga tani 50.7, Soya tani 134.56 na Mbaazi tani 46.4 na kwamba Msimu wa 2016/2017 wakulima walitumia pembejeo kiasi cha tani 19,450 za mbolea, kati ya hizo mbolea tani 173.8 zilikuwa ni za ruzuku ya Serikali.
Hata hivyo amesema Pembejeo hizo zilitumika Katika mazao ya mahindi, kahawa na mpunga ambapo Halmashauri ina maduka ya pembejeo za kilimo 45 na kampuni tano ya pembejeo.Amesema hali ya zana za kilimo za kisasa katika Halmashauri imeendelea kuboreshwa kwa wakulima mmoja mmoja na kwenye vikundi kwa kununua na kukopa matrekta 143 madogo na makubwa ambayo yanatumika kuongeza tija katika kilimo.
Akizungumzia kuhusu kilimo cha umwagiliaji,Mkurugenzi huyo amelitaja eneo linalofaa kwa kilimo cha umwagiliaji kuwa ni la ukubwa wa hekta.2,000,kati ya hizo hekta 195 ndio zinalimwa sawa na asilimia 9.7. na kwamba hadi sasa kuna skimu tatu za umwagiliaji ambazo miundo mbinu yake imejengwa na zinafanya uzalishaji wa tani 375 za mpunga na tani 113 za viazi vitamu.
Imetolewa na Albano Midelo
Afisa Habari Manispaa ya Songea
Agosti 24,2018
SONGEA MUNICIPAL COUNCIL
Anuani ya Posta: P O BOX 14, SONGEA
Simu ya Mezani: 025 2602970
Simu ya Kiganjani:
Barua Pepe: info@songeamc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Manispaa ya Songea. Haki zote zimehifadhiwa