MKOA wa Ruvuma unatajwa kuwa miongoni mwa mikoa mitano nchini ambayo inaongoza kwa utapiamlo na udumavu nchini.
Takwimu za Wizara ya Afya zilizotolewa mwaka 2017/2018 zinaonesha kuwa udumavu katika Mkoa wa Ruvuma ni asilimia 44 licha ya kwamba Mkoa unaongoza kwa uzalishaji wa mazao ya chakula.
Kufuatia hali hiyo ipo haja ya kuwa na mikakati ya kujikwamua katika tatizo la udumavu.Moja ya mikakati hiyo ni kuundwa kwa Kamati za lishe katika kila Halmashauri nchini ambazo zinakutana kila baada ya miezi mitatu.
Kamati ya Lishe ya Halmashauri ya Manispaa ya Songea ikiongozwa na Mwenyekiti wake Devota Luwungo imebainisha mikakati mbalimbali iliyochukuliwa ili kukamiliana na udumavu ikiwemo kutoa elimu kupitia vyombo vya habari,vipeperushi na mitandao ya kihabari.
Taarifa ya utekelezaji wa shughuli za lishe katika Idara ya Afya katika kipindi cha Aprili hadi Juni 2019 inaonesha kuwa asilimia nne ya watoto chini ya miaka mitano wana hali duni ya lishe ikilinganishwa na asilimia 5.4 ya kipindi cha Januari hadi Machi 2019.
Kulingana na taarifa hiyo,jumla ya akinamama 7821 walihudhuria kliniki kati ya hao 7758 walipata madini ya chuma sawa na asilimia 99.2 na akinamama wajawazito 1914 walipata dawa za minyoo kati 1926 waliotakiwa kupata sawa na asilimia 99.4.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo katika kipindi hicho watoto hai waliozaliwa ni 2873 kati yao watoto 304 walibainika kuzaliwa na uzito pungufu wa kilo 2.5 sawa na asilimia 10.6.
Utafiti uliofanyika katika mitaa 95 iliyopo ndani ya Halmashauri ya Manispaa ya Songea ,umebaini kuwa asilimia 86.43 ya kaya zilizopo katika mitaa hiyo zina vyoo bora na asilimia 48.12 ya kaya hizo zina miundombinu ya kunawa mikono nje ya choo na asilimia 87 ya kaya hizo zina maji safi na salama.
Imeandikwa na Albano Midelo
Afisa Habari Manispaa ya Songea
Septemba 3,2019
SONGEA MUNICIPAL COUNCIL
Anuani ya Posta: P O BOX 14, SONGEA
Simu ya Mezani: 025 2602970
Simu ya Kiganjani:
Barua Pepe: info@songeamc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Manispaa ya Songea. Haki zote zimehifadhiwa