Na,
AMINA PILLY,
AFISA HABARI MANISPAA.
13.01.2022
Halmashauri ya Manispaa ya Songea yajipanga kuanza kutumia mfumo wa hati fungami kwa lengo la utekelezaji wa miradi ya kimkakati, kiuchumi na kijamii.
Hayo yamebainishwa katika mafunzo yaliyotolewa na viongozi wa soko la hisa kwa watalaamu, viongozi pamoja na wadau mbalimbali hapo jana 13 Januari 2022 katika ukumbi wa Manispaa ya Songea kwa lengo la kujenga uelewa juu ya matumizi ya hati fungani za Serikali za mitaa nchini Tanzania.
Akizungumza katika mafunzo hayo mgeni rasmi ambaye alikuwa ni Katibu Tawala Mkoa wa Ruvuma Steven Ndaki alisema kuwa hati fungani za Serikali za mitaa ni dhamana inayohusisha mikopo kwa Halmashauri ambayo itasaidia kupata fedha zitakazotumika katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo, ambayo yatasaidia katika utekelezaji wa muongozo wa uwekezaji ulioandaliwa mwaka 2019 na Mkoa wa Ruvuma kwa Halmashauri zote 8 kwa lengo la kukuza uchumi wa Halmashauri na Mkoa kwa ujumla.
“Muongozo huo wa uwekezaji unaangalia maeneo mbalimbali ikiwemo na uwekezaji katika eneo la kilimo, ujenzi wa miundombinu bora, ufugaji pamoja na kuwekeza katika majengo makubwa ya biashara “Alibainisha.
Kwa upande wake Afisa Mtendaji Mkuu wa soko la Hisa la Dar es salaam Moremi Marwa alisema kuwa lengo la kutoa mafunzo hayo ni utekelezaji wa agizo la Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan lililotolewa Oktoba 2021 kwa Wizara ya Fedha na Wizara ya Tamisemi kushirikiana na soko la Hisa kwa lengo la kuwezesha Halmashauri kupata fedha ambazo zitasaidia kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo kwenye Halmashauri nchini.
Alisema kuwa soko la Hisa lipo tayari kutoa ushirikiano kwa Halmashauri ya Manispaa ya Songea ili kufanikisha uwekezaji wa miradi mbalimbali kama ilivyobainishwa katika muongozo wa uwekezaji uliotolewa na viongozi wa Mkoa wa Ruvuma.
Akieleza Mkurugenzi wa Biashara katika Soko la Hisa Dar es salaam Ibrahim Mshindo alisema kuwa lengo la mfumo wa hati fungani ni kurahisisha shughuli za uwekezaji kwa Serikali kuu, Taasisi binafsi, wafanyabiashara pamoja na Serikali za mitaa ili kuleta maendeleo kwa kupata mkopo wenye riba nafuu.
Aidha, Afisa biashara wa Manispa ya Songea Furaha Mwangakala alibinisha kuwa Manispaa ya Songea ina fursa nyingi za uwekezaji ikiwemo na maeneo kwa ajili ya viwanda vidogo na vikubwa, kilimo, ufugaji na biashara,
Naye Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Songea Dkt. Frederick Sagamiko alisema kuwa Manispaa ya Songea imejipanga kushirikaiana na sekta binafsi na wadau mbalimbali ikiwemo na wafanyabiashara kwa lengo la kuongeza wawekezaji na kufikia malengo ya kutoka kwenye hadhi ya Manispaa na kuwa Jiji.’Alieleza’
Vilevile, Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Hamisi Abdallah Ally amelitaka Baraza la Madiwani Manispaa ya Songea kufanyia kazi na kupitisha mpango wa matumizi ya hati fungani za Serikali za Mitaa ndani ya Halmashauri ili kuweza kuleta maendeleo kwa wananchi.
Akifunga mafunzo hayo, Mstahiki Meya Manispaa ya Songea Michael Mbano, kwa niaba ya Katibu Tawala Mkoa wa Ruvuma, ametoa wito kwa wataalamu kushirikiana na wafanyabiashara pamoja na sekta binafsi ili kuleta maendeleo katika Halmashauri ya Manispaa ya Songea.
Mwisho.
SONGEA MUNICIPAL COUNCIL
Anuani ya Posta: P O BOX 14, SONGEA
Simu ya Mezani: 025 2602970
Simu ya Kiganjani:
Barua Pepe: info@songeamc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Manispaa ya Songea. Haki zote zimehifadhiwa