HALMASHAURI ya Manispaa ya Songea mkoani Ruvuma imejipanga kupima maeneo mbalimbali kwa kupanga matumizi kulingana na mahitaji ya sasa.
Kwa kuanzia Halmashauri imepanga eneo la Kata ya Lilambo kwa matumizi ya viwanda vidogo ,vya kati na vikubwa na kwamba katika eneo hilo pia kuna maeneo ya maegesho,soko,kituo cha mafuta,makazi na biashara.
Upimaji wa eneo hilo umekwaishaanza ambapo hadi kufikia Agosti mwaka huu zaidi ya viwanja 70 vilikuwa vimepimwa kati ya viwanja 250 ambavyo vinatarajiwa kupimwa.
Hata hivyo katika upimaji unaoendelea,viwanja vinapimwa katika maeneo ambayo yamelipwa fidia tu ambapo Halmashauri ya Manispaa ya Songea imelipa zaidi ya shilingi milioni 47 kati ya shilingi milioni 233.84 zinazotakiwa kulipwa katika viwanja vyote ili viweze kupimwa.
Viwanja ambavyo vimepimwa vipo katika hatua ya mahesabu tayari kupelekwa kwa Mkurugenzi wa Upimaji kwa ajili ya usajili ambapo Halmashauri inaendelea na urasimishaji wa maeneo mbalimbali ya Halmashauri kwa kushirikiana na Wizara ya Ardhi,Nyumba na Maendeleo ya Makazi.
Halmashauri ya Manispaa ya Songea inaendelea na mpango wake wa kupima viwanja 6000 katika kipindi cha miezi mitatu katika maeneo ya Makambi,Matogoro,Mkwawa,Chemchem,Seedfarm,Kuchile,Making’inda,Miembeni,Mjimwema,Luwawasi,Ruhuwiko na Ruvuma.
Upimaji katika maeneo hayo unaendelea ambapo hadi sasa viwanja zaidi ya 2805 vimekwishapimwa na kwamba Halmashauri imejipanga kufanya zoezi hili liwe endelevu hasa katika maeneo yote yalioiva kama Mitawa,Shule ya Tanga,Subira na Mletele.
Katika Mpango Mkakati huo Halmashauri imelazimika kushirikiana na wananchi kupima kwa sababu Halmashauri haina fedha za kulipa fidia hali inayosababisha kukosa viwanja vyake yenyewe na badala yake kuwapimia wananchi kwa makubaliano ya kulipa shilingi kati ya 80,000 hadi 100,000 kwa kila kiwanja ili kuondoa makazi holela katika Mji wa Songea.
Imetolewa na Albano Midelo
Afisa Habari Manispaa ya Songea
Septemba 3,2018
SONGEA MUNICIPAL COUNCIL
Anuani ya Posta: P O BOX 14, SONGEA
Simu ya Mezani: 025 2602970
Simu ya Kiganjani:
Barua Pepe: info@songeamc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Manispaa ya Songea. Haki zote zimehifadhiwa