HALMASHAURI ya Manispaa ya Songea mkoani Ruvuma imetoa mkopo wa zaidi ya milioni 61 katika vikundi 48 vya wajasirimali wadogo.
Akisoma taarifa ya utoaji mikopo kwa vikundi vya wanawake,vijana na makundi maalum kwenye ukumbi wa Manispaa ya Songea,Mkuu wa Idara ya Maendeleo ya Jamii,Naftari Saiyoloi amesema fedha hizo zimetokana na mapato ya ndani ya asilimia kumi.
Amesema fedha zinazokopeshwa ni mapato ya ndani ya shilingi milioni 40 na fedha za marejesho ya mikopo ambazo ni shilingi milioni 21 na kwamba mikopo inatolewa ili kukamilisha utoaji wa mikopo ya robo ya mwaka wa fedha wa 2018/2019.
“Katika mwaka wa fedha wa 2017/2018 jumla ya vikundi vya wanawake 127 vimekopeshwa shilingi milioni 33.9 hivyo kufanya jumla ya fedha zilizokopeshwa kufikia milioni 196’’,alisisitiza Saiyoloi.
Mgeni rasmi katika hafla hiyo Mkuu wa Wilaya ya Songea Pololet Mgema amesema serikali imekwishaagiza kuanzia mwaka wa fedha wa 2018/2019 hakutakuwepo tena na tozo ya riba ya asilimia 10 kama ilivyokuwa katika miaka ya nyuma.
“Fedha hizi mnaazimwa mkazifanyie kazi na baadaye mzirejeshe,fedha hizi ni za kwenu wanawake,vijana na makundi maalum waliopo katika Halmashauri ya Manispaa ya Songea,tunapeana kwa zamu’’,alisisitiza
Hata hivyo Mkuu wa Wilaya ameagiza wale wote waliopewa mikopo kuirejesha kwa wakati ili zitumike kuwakopesha wajasirimali wadogo wengine na kufanya biashara yenye tija kwa kuwa na mkopo mkubwa.
Ameitaja azma ya serikali kuwa na mfuko mkubwa wa kukopesha wajasirimali wadogo hali ambayo itasababisha kutokuwa na sababu tena ya kutenga bajeti.
Halmashauri ya Manispaa ya Songea katika kipindi cha mwaka wa fedha wa 2018/2019 imeweza kutoa mikopo kwa wanawake,vijana na makundi maalum kwa asilimia 91.
Imeandikwa na Albano Midelo
Afisa Habari Manispaa ya Songea
Juni 20,2019
SONGEA MUNICIPAL COUNCIL
Anuani ya Posta: P O BOX 14, SONGEA
Simu ya Mezani: 025 2602970
Simu ya Kiganjani:
Barua Pepe: info@songeamc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Manispaa ya Songea. Haki zote zimehifadhiwa