Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Christina Mndeme ameipongeza Halmashauri ya Manispaa ya Songea kwa kufikisha asilimia 90 katika ukusanyaji wa mapato ya ndani hadi kufikia Juni 2019.
Mndeme ametoa pongezi hizo wakati anazungumza katika kikao maalum cha Baraza la madiwani cha kujadili taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali katika kipindi cha mwaka 2017/2018 kwenye ukumbi wa Manispaa ya Songea.
“Niwapongeze waheshimiwa madiwani,Mkuu wa Wilaya,Mkurugenzi ,wataalam na wadau wengine kwa kuiwezesha Halmashauri ya Manispaa ya Songea kututoa kimasomaso katika ukusanyaji wa mapato ya ndani kwa zaidi ya asilimia 90’’.alisisitiza.
Mndeme pia ameipongeza Halmashauri ya Manispaa ya Songea kwa kuweza kuchangia asilimia 100 katika mfuko wa wanawake na vijana na kuweza kuchangia zaidi ya shilingi milioni 176.25 katika mwaka wa fedha wa 2018/2019.
Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma ameipongeza Manispaa ya Songea kwa kuweza kudumu katika hati safi katika kipindi cha miaka mitatu mfululizo kuanzia mwaka 2015/2016,2016/2017 na 2017/2018.
Amesema kitendo hicho ni matokeo ya utendaji kazi mzuri wenye mshikamano na ushirikiano kati ya wataalam wa Halmashauri,Mkurugenzi na waheshimiwa madiwani.
Hata hivyo Mndeme amekumbusha kuwa kupata hati safi kusiwafanye watendaji katika Manispaa hiyo kubweteka na kuona wamefika mwisho,badala yake uwe mwanzo wa kujiandaa na ukaguzi katika mwaka mwingine wa fedha.
“Katika Manispaa ya Songea kuna hoja na mapendekezo ya Mdhibiti na Mkaguzi wa Hesabu za Serikali zinazofikia 33 ambazo zinatakiwa kujadiliwa na kuwasilishwa kwa ajili ya uhakiki na hatimaye kufungwa.
Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali hufanya ukaguzi baada ya mwaka wa fedha kufungwa.
Imeandikwa na Albano Midelo
Afisa Habari Manispaa ya Songea
Juni 28,2019
SONGEA MUNICIPAL COUNCIL
Anuani ya Posta: P O BOX 14, SONGEA
Simu ya Mezani: 025 2602970
Simu ya Kiganjani:
Barua Pepe: info@songeamc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Manispaa ya Songea. Haki zote zimehifadhiwa