Manispaa ya Songea yapanda miche ya miti 6200
HALMASHAURI ya Manispaa ya Songea mkoani Ruvuma imeadhimisha siku ya upandaji miti kitaifa Januari 24 kwa kupanda miche ya miti 6200 katika chanzo cha maji Namanditi.
Wananchi wa Kata ya Ruhuwiko wakiongozwa na madiwani wa Manispaa ya Songea walishiriki kupanda miche ya miti ya asili.Mgeni rasmi katika zoezi hilo alikuwa ni Mstahiki Meya wa Manispaa ya Songea Alhaj Abdul Hassan Mshaweji.
Awali akitoa taarifa ya Idara ya Maliasili Katika Manispaa ya Songea,Mkuu wa Idara hiyo Godfrey Luhimbo alizitaja shughuli za kibinadamu kuwa ndiyo chanzo kikuu cha uharibifu wa mazingira ambapo katika Manispaa ya Songea uharibifu aliutaja kuwa unatokana na uvamizi wa misitu ya hifadhi.
Sababu nyingine alizitaja kuwa ni ukataji miti hovyo kwenye vyanzo vya maji na kwenye misitu ya hifadhi kwa lengo la kuzalisha mazao ya misitu kama vile mkaa,nguzo,kuni na mbao na uwindaji wa wanyama
“Kutokana na uharibifu wa mazingira tunakabiliwa na changamoto nyingi zikiwemo kuongezeka kwa joto la dunia,unyeshaji wa mvua usiokuwa na mpangilio,ukame na maradhi mbalimbali yanayomkabili binadamu’’,alisisitiza.
Katika kukabilina na changamoto hizo ameitaja mikakati inayofanywa na Idara ya Maliasili kuwa ni kutoa elimu,kupanda miti kila mwaka katika maeneo mbalimbali na kufanya doria za mara kwa mara ili kudhibiti uharibifu wa misitu.
Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Songea Naftari Saiyoloi amewaasa wakazi wa Namanditi kuhakikisha miche ya miti iliyopandwa inatunzwa ili iweze kukua na kusaidia kuimarisha vyanzo vya maji ambavyo ni muhimu kwa maendeleo endelevu.
Naye mgeni rasmi Mstahiki Mstahiki Meya wa Manispaa ya Songea Alhaj Abdul Hassan Mshaweji amewaasa wananchi wa Songea na watanzania kwa ujumla kulinda miti ambayo ni muhimu ikiwemo dawa.
“Binadamu anaongoza kwa kuharibu misitu,Mwenyezi Mungu amevileta vitu vyote duniani vinatakiwa vitunzwe,ikiwemo mimea ambayo ni muhimu kwa mazingira endelevu’’,alisema Mshaweji.
Ametoa rai kwa wananchi kuendelea kutunza na kuvilinda vyanzo vya maji vilivyopo ili kuepukana na madhara ya uharibifu wa mazingira ikiwemo ukame ambao unaweza kusababisha viumbe hai kushindwa kuishi.
Imeandikwa na Albano Midelo
Afisa Habari Mkoa wa Ruvuma
Januari 24,2020
SONGEA MUNICIPAL COUNCIL
Anuani ya Posta: P O BOX 14, SONGEA
Simu ya Mezani: 025 2602970
Simu ya Kiganjani:
Barua Pepe: info@songeamc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Manispaa ya Songea. Haki zote zimehifadhiwa