Manispaa ya Songea yapata Naibu Meya mpya
HALMASHAURI ya Manispaa ya Songea iliyopo katika mkoa wa Ruvuma Agosti 2017 imepata Naibu Meya mpya.
Mheshimiwa Yobo Mapunda ambaye ni Diwani wa Kata ya Lilambo amechaguliwa kuwa Naibu Meya wa Manispaa ya Songea baada ya kuchaguliwa kwa kura za ndiyo 22 kati ya kura 27 zilizopigwa.
Yobo amepata ushindi mkubwa wa asilimia 92 ambapo alipata kura tano za hapana sawa na asilimia nane.
Uchaguzi wa kumchagua Naibu Meya umefanyika katika mkutano wa kufunga mwaka na kuanza mwaka mpya wa serikali wa Baraza la Madiwani la Manispaa hiyo uliofanyika kwenye ukumbi wa Manispaa ya Songea.
Mkutano huo ulifunguliwa na Mkuu wa Wilaya ya Songea Pololet Kamando Mgema ambaye pamoja na mambo mengine aliwapongeza madiwani hao kwa kufanikisha kero mbalimbali zilizokuwa zinawakabili wananchi katika kata zao.
Mheshimiwa Yobo amechukua nafasi ya Mheshimiwa Consolata Chilowoko ambaye ameng'atuka baada ya kumaliza muda wake kisheria wa kuwa Naibu Meya wa Manispaa hiyo.
Akizungumza baada ya kuchaguliwa Yobo amesema yupo tayari kushirikiana kwa karibu na Mstahiki Meya wa Manispaa ya Songea Alhaji Abdul Hassan Mshaweji ili kuhakikisha wanajenga manispaa ya Songea ambayo inajiandaa na safari ya kuwa Jiji.
Amesema katika kipindi chake cha uongozi atawaunganisha watalaam wa Manispaa ya Songea na madiwani wote ili kumaliza tofauti zilizokuwepo awali ambazo zilikuwa zinarudisha nyuma maendeleo ya Manispaa hiyo kutokana na migogoro katika utendaji baina ya madiwani na watalaam.
SONGEA MUNICIPAL COUNCIL
Anuani ya Posta: P O BOX 14, SONGEA
Simu ya Mezani: 025 2602970
Simu ya Kiganjani:
Barua Pepe: info@songeamc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Manispaa ya Songea. Haki zote zimehifadhiwa