HALMASHAURI ya Manispaa ya Songea mkoani Ruvuma ina jumla ya viwanja 35,500 vilivyopimwa katika maeneo mbalimbali ya Manispaa hiyo.
Mkurugenzi wa Manispaa hiyo Tina Sekambo amesema Kati ya hivyo viwanja 18,489 ramani zake zimesajiliwa na kwamba maeneo ambayo ramani zake hazijasajiliwa yameundiwa kamati Kwa kuwashirikisha Wananchi ili kukamilisha Upimaji kwa njia ya Upimaji shirikishi.
“Halmashauri imetekeleza agizo la serikali kwa kuhakikisha maeneo yote ya umma yanapimwa na kuandaliwa hati. Maeneo hayo yanajumuisha vituo vya afya, Maneo ya shule za Msingi na Sekondari, Zahanati pamoja na Ofisi za Umma’’,alisema.
Hata hivyo Sekambo amesema, hadi sasa jumla ya maeneo 170 yamepimwa na mengine yamepimwa kwa hatua ya awali (Demarcation) na mchakato wa kukamilisha upimaji huo unafanyika na ramani hizo zinasajiliwa.
Kulingana na Mkurugenzi huyo,Halmashauri ya Manispaa ya Songea,imeandaa Mpango kabambe (MasterPlan) ambao umeidhinishwa na Wizara na utatumika katika kipindi cha miaka 20 (2017-2037) kama dira ya maendeleo ya Mji wa Songea.
Amesema Katika mpango huo, Halmashuri imetenga matumizi mbalimbali ambayo yataleta tija katika Mji wa Songea ikiwemo maeneo ya viwanda katika kata ya Lilambo, Mletele, Tanga na Eneo la Uwekezaji EPZA Mwengemshindo lenye jumla ya hekari 5000.
Ameongeza kuwa Halmashauri hiyo imetenga na kupima eneo la ekari 170 lililopo katika Kata ya Lilambo kwa matumizi ya Viwanda.
Kuhusu makisio ya ukusanyaji wa Pango la Kodi ya Ardhi kwa mwaka wa fedha 2018/2019,Sekambo amesema Manispaa ya Songea ilipangiwa kukusanya jumla ya sh.milioni 600 ambapo hadi sasa zimekusanywa sh.milioni 316 toka kwa wamiliki wa viwanja mbalimbali na kwamba wananchi 274 wamefikishwa Mahakamani kwa kukaidi kulipa kodi ya pango la ardhi.
Imeandaliwa na Albano Midelo
Afisa Habari Manispaa ya Songea
SONGEA MUNICIPAL COUNCIL
Anuani ya Posta: P O BOX 14, SONGEA
Simu ya Mezani: 025 2602970
Simu ya Kiganjani:
Barua Pepe: info@songeamc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Manispaa ya Songea. Haki zote zimehifadhiwa