HALMASHAURI ya Manispaa ya Songea mkoani Ruvuma Septemba 13,2018 imesaini mikataba minne ukiwemo mkataba wa uendeshaji wa Bustani ya Manspaa ya Songea ambao umesainiwa baina ya Halmashauri ya Manispaa na Mwendeshaji aliyeshinda zabuni anayeitwa Neema Kajange.
Hafla ya kusaini mikataba hiyo imefanyika katika ofisi ya Mstahiki Meya wa Halmashauri ya Manispaa ya Songea Alhaj Abdul Hassani Mshaweji mbele ya wanahabari.
Mkataba wa uendeshaji wa bustani ya Manispaa ya Songea ni wa shilingi milioni 15 ambao utafanyika katika kipindi cha miezi kumi ambapo Mwekezaji ataendesha shughuli mbalimbali ikiwemo hoteli,choo na mchezo wa bembea.
Kwa mujibu wa Mwekezaji,bustani hiyo inafunguliwa rasmi Jumatatu ya Septemba 17,2018 na kwamba uzinduzi rasmi wa bustani unatarajia kufanyika Oktoba 27,mwaka huu katika viwanja vya bustani hiyo.
Mkataba wa pili ambao umesainiwa baina ya Halmashauri ya Manispaa ya Songea na Kampuni ya STUMAK ENGINEERING CO.LTD ya Songea unahusu ujenzi wa kituo cha kutolea huduma za afya(CTC) katika kituo cha afya Mjimwema.Mkataba huo ni wa siku 30 wenye thamani ya shilingi milioni 29,673,311.32.
Mkataba wa tatu ni wa ununuzi wa mashine ya kuchapisha ramani (PLOTTER MACHINE) ambao umesainiwa baina ya Halmashauri ya Manispaa ya Songea na Kampuni ya DON TECHNOLOGIES LTD ya Songea kwa siku 45 wenye thamani ya shilingi milioni 28,900,000.00
Mkataba wa nne ambao umesaini ni kati ya Halmashauri ya Manispaa ya Songea na Robert Mgowole unaohusu uendeshaji wa choo cha soko la Manzese B wenye thamani ya shilingi milioni 3,600,00.00 katika kipindi cha miezi 10.
Akizungumza mara baada ya kusainiwa kwa mikataba hiyo,Mstahiki Meya wa Manispaa ya Songea Alhaj Abdul Hassan Mshaweji amewaasa wote waliosaini mikataba hiyo kufanyakazi kwa ufanisi kwa sababu Manispaa ya Songea hivi sasa ipo katika mchakato wa kutoka katika Halmashauri ya Manispaa ya kuingia katika Halmashauri ya Jiji.
Imetolewa na Albano Midelo
Afisa Habari Manispaa ya Songea
Septemba 13,2018
SONGEA MUNICIPAL COUNCIL
Anuani ya Posta: P O BOX 14, SONGEA
Simu ya Mezani: 025 2602970
Simu ya Kiganjani:
Barua Pepe: info@songeamc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Manispaa ya Songea. Haki zote zimehifadhiwa