Na,
AMINA PILLY,
AFISA HABARI MANISPAA.
02.12.2021
Mkuu wa Wilaya ya Songea Pololet Kamando Mgema amewaongoza wakazi wa Manispaa ya Songea katika kuadhimisha siku ya UKIMWI Duniani ambayo huadhimishwa duniani kote kila ifikapo tarehe 01 Disemba ya kila mwaka.
Maadhimisho hayo yamefanyika katika uwanja wa Nane nane Manispaa ya Songea hapo jana tarehe 01 Disemba 2021 na kuhudhuriwa na wadau mbalimbali wakiwemo na INTER CARE, PADI, KONGA, na wananchi kwa lengo la kutoa fursa ya kutafakari kwa mara nyingine kuhusu tulikotoka, tulipo na tunakokwenda katika mapamabano dhidi ya VVU na UKIMWI kwenye Halmashauri na Taifa kwa ujumla.
Pololet alisema Maadhimisho ya siku ya UKIMWI duniani hutumika kwa kuwakumbuka kwa huzuni ndugu zetu waliopoteza maisha wahanga wa mwanzo wa kuenea kwa VVU na UKIMWI wakati ambao hapakuwepo na huduma stahiki za matibabu ya kufubaza Virus vya UKIMWI.
Aliongeza kuwa tunakumbushwa kuendelea kujikinga dhidi ya maambukizi ya VVU na UKIMWI na kuwakinga na wengine, pia kwa wale waliokutwa na maambukizi wanatakiwa kuanza tiba mara moja ikiwemo na kuanza dawa mapema.
Amewataka wananchi kupima na kutambua afya zao kwa hiari kwasababu endapo utapima VVU na utakutwa na maambukizi utaunganishwa mapema katika huduma ya tiba ya kufubaza VVU na kuweza kuimarisha afya pamoja na kuchukua tahadhari kwa kuacha tabia hatarishi zinazoweza kueneza maambukizi ya VVU katika jamii.’Alibainisha’
Ametoa wito kwa wadau wote kuendelea kutoa mchango ili kupambana na VVU pamoja na wataalamu kutenga bajeti kwa ajili ya kamati za mitaa na kata ili kupambana na maambuki ya VVU.
Ametoa rai kwa wananchi kuendelea kuishi kwa tahadhari dhidi ya magonjwa ya mlipuko hasa ugonjwa wa UVIKO-19 kwa kuendelea kupata chanjo ambayo inatolewa bure katika vituo mbalimbali vya afya ndani ya Manispaa ya Songea.’Pololet alisisitiza’
Kwa upande wake Mratibu wa UKIMWI tiba Manispaa ya Songea Felista Kibena alisema kuwa huduma ya upimaji VVU inaendelea kutolewa katika vituo vya kutoa huduma ya afya na kwenye jamii na katika kipindi cha mwaka wa fedha Julai 2020 hadi Juni 2021 jumla ya watu 48240 walipima afya zao (wanaume 22715 na wanawake 26525) ambapo kati ya hao wanaume 792 na wanawake 1160 walikutwa na maambukizi ya VVU ambayo ni sawa na asilimia 4.0%, na wote walifanikiwa kuunganishwa kwenye huduma ya tiba na matunzo katika vituo vya CTC.
Naye Mratibu wa UKIMWI kinga Manispaa ya Songea Humphrey Mbawala alieleza kauli mbiu ya maadhimisho ya siku ya UKIMWI duniani kwa mwaka 2021 ambayo ni “Zingatia usawa, Tokomeza UKIMWI, Tokomeza magonjwa ya mlipuko”
Alibainisha kuwa kauli mbiu hiyo inalenga kuhamasisha Serikali, wananchi, Taasisi, Asasi, makampuni na makundi mbalimbali ya jamii kushiriki kikamilifu katika kudhibiti VVU/UKIMWI pamoja na magonjwa ya mlipuko kama UVIKO-19 nchini ili kuweza kwenda sawa na mtazamo wa kimataifa wa kumaliza maambukizi ifikapo mwaka 2030.
Miongoni mwa mikakati iliyowekwa na Manispaa ya Songea ni pamoja na kuendelea kuwasaidia watoto wenye mahitaji maalumu ambapo katika maadhimisho hayo ziliandaliwa zawadi zilizotolewa kwa watoto 25 wenye mahitaji maalumu kutoka kwenye mitaa mbalimbali ndani ya Manispaa ya Songea zenye thamani ya shilingi 1,000,000/= kwa ajili ya kuwafariji watoto hao, ambapo vifaa hivyo vilivyotolewa ni pamoja na mchele, sabuni, sare za shule, mafuta ya kupaka, begi la shule na daftari.
Katika kuadhimisha siku ya UKIMWI duniani hapo jana Halmashauri ya Manispaa ya Songea iliandaa vibanda mbalimbali kwa lengo la kutoa huduma ya ushauri nasaha na kupima VVU kwa hiari pamoja na utoaji wa chanjo ya UVIKO-19 ambapo jumla ya watu 54 walijitokeza kupima afya zao kati yao wanaume 34 na wanawake 20 na wote wakagundulika kuwa hawana maambukizi ya VVU na watu 28 (wanaume 14 n wanawake 14) walijitokeza kupata chanjo ya UVIKO-19 kwa hiari.
Mwisho.
SONGEA MUNICIPAL COUNCIL
Anuani ya Posta: P O BOX 14, SONGEA
Simu ya Mezani: 025 2602970
Simu ya Kiganjani:
Barua Pepe: info@songeamc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Manispaa ya Songea. Haki zote zimehifadhiwa