HALMASHAURI ya Manispaa ya Songea katika kipindi cha mwaka 2018/2019 imetenga shilingi milioni 150 kwa ajili ya ujenzi wa zahanati,ununuzi wa vifaa vya afya na ujenzi wa nyumba za watumishi wa afya.
Mkurugenzi wa Manispaa ya Songea Tina Sekambo amesema Mpaka kufikia Machi,2019 zaidi ya shilingi milioni 58 zimepelekwa katika kutekeleza miradi mbalimbali ya afya.
Ameitaja miradi hiyo kuwa ni ujenzi wa zahanati ya makambi katika kata ya Ndilimalitembo,ujenzi wa zahanati ya Sinai katika kata ya Lilambo,ujenzi wa Zahanati ya Lupapila katika kata ya Subira na ujenzi wa Zahanati ya Seedfarm katika kata ya Seedfarm.
Katika hatua nyingine Sekambo amesema Halmashauri imeendelea kuhakikisha upatikanaji wa chanjo mbali mbali za watoto na mama wajawazito kama vile chanjo za kukinga kifua kikuu, ugonjwa wa kupooza, kukinga magojwa ya pepopunda, donda koo, homa ya ini na kifaduro,Vichomi, uti wa mgongo, na Surua.
“Hali ya utoaji wa chanjo ni nzuri kwani chanjo ya Penta 3 ambayo ndiyo kigezo cha mpango wa chanjo kitaifa tumefikia asilimia 96.2, lengo la kitaifa ni kufikia asilimia 90. Kiwango cha utapiamlo mkali ni asilimia 0.1 na utapia mlo usio mkali ni asilimia 4.1’’,alisema Sekambo .
Hata hivyo amesema Kuanzia mwanzoni mwa Januari 2018 hadi sasa hakuna upungufu wa chanjo katika Halmashauri ya Manispaa ya Songea.
Imeandikwa na Albano Midelo
Afisa Habari Manispaa ya Songea
Aprili 18,2019
SONGEA MUNICIPAL COUNCIL
Anuani ya Posta: P O BOX 14, SONGEA
Simu ya Mezani: 025 2602970
Simu ya Kiganjani:
Barua Pepe: info@songeamc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Manispaa ya Songea. Haki zote zimehifadhiwa